Michezo

Rodrygo asaidia Real Madrid kuangusha Inter Milan

November 4th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

BAO la dakika za mwisho kutoka kwa Rodrygo liliwavunia Real Madrid ushindi wa 3-2 dhidi ya Inter Milan kwenye gozi la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Novemba 3, 2020.

Huo ulikuwa ushindi wa kwanza kwa miamba hao wa soka ya Uhispania kusajili hadi kufikia sasa kwenye kampeni za UEFA msimu huu.

Real walitwaa udhibiti wa mchuano huo baada ya fowadi Karim Benzema kuwaweka kifua mbele kunako dakika ya 25 kabla ya nahodha Sergio Ramos kufunga goli la pili katika dakika ya 33 baada ya kumzidi maarifa kipa Samir Handanovic. Bao la Ramos lilikuwa lake la 100 akivalia jezi za kikosi cha Real ambacho sasa kinatiwa makali na kocha Zinedine Zidane.

Inter walirejea mchezoni dakika chache baadaye kupitia kwa Lautari Martinez aliyeshirikiana vilivyo na Nicolo Barella katika dakika ya 35. Ivan Perisic alisawazisha mambo kunako dakika ya 68 baada ya kupokezwa krosi safi kutoka kwa Martinez ambaye anahusishwa pakubwa na uwezekano wa kuhamia Barcelona ya Uhispania.

Rodrygo ndiye aliyeibuka mfalme wa mechi hiyo hatimaye kwa kuwafungia Real bao la ushindi baada ya kujaza kimiani krosi aliyoandaliwa na Vinicius Jr katika dakika ya 80.

Ushindi kwa Real unawasaza kundini na alama nne sawa na Shakhtar Donetsk ambao wanashikilia nafasi ya pili. Ni pengo la alama moja ndilo linalotamalaki kati ya vikosi hivyo viwili na viongozi Borussia Monchengladbach kutoka Ujerumani. Inter ya kocha Antonio Conte inakokota nanga mkiani kwa alama mbili pekee.

M’gladbach iliwapokeza Shakhtar kichapo cha 6-0, ushindi uliomshuhudia nyota Alassane Plea akifunga mabao matatu ambayo ni yake ya kwanza kwenye kivumbi cha UEFA.

Real ambao ni mabingwa mara 13 wa UEFA, walishuka dimbani kwa minajili ya mechi dhidi ya Inter wakivuta mkia wa kundi lao baada ya kupigwa 3-2 na Shakhtar kisha kuambulia sare ya 2-2 dhidi ya M’gladbach katika mechi mbili za kwanza.

Walitawaliwa na kiu ya kukomesha rekodi mbovu iliyowashuhudia wakikosa kusajili ushindi katika mechi nne zilizopita za UEFA ikiwemo ile iliyowapa Manchester City fursa ya kuwabandua kwenye hatua ya 16-bora msimu uliopita wa 2019-20.

Real kwa sasa wameshinda mechi saba kati ya nane ambazo zimewakutanisha na Inter katika uwanja wao wa nyumbani.