Roho mkononi Simbas wakisubiri kambi ya mazoezi raga SA

Roho mkononi Simbas wakisubiri kambi ya mazoezi raga SA

NA GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji 15 kila upande almaarufu Kenya Simbas ina mipango ya kujipiga msasa nchini Afrika Kusini mwezi Oktoba kwa mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia.

Kocha Paul Odera alieleza Taifa Spoti kuwa wamekamilisha kuandika bajeti na kufanya mipango, ingawa roho iko mkononi ikisubiri udhamini wa kambi hiyo ambao bado haujathibitishwa.

Mabingwa wa zamani wa Afrika Kenya (nambari 33 duniani) wameratibiwa kumenyana na Amerika (19), Ureno (20) na Hong Kong (22) mnamo Novemba 6, 12 na 18 mjini Dubai katika mashindano ya mwisho ya kuingia Kombe la Dunia 2023.

Mshindi kutoka orodha ya mataifa hayo manne ataingia Kundi C kupepetana na Wales, Australia, Fiji na Georgia. Simbas walijipata katika mchujo huo walipozidiwa ujanja na Namibia katika fainali ya Kombe la Afrika 36-0 nchini Ufaransa mwezi Julai.

Namibia walifuzu moja kwa moja, wakiingia Kundi A lililo na New Zealand, Ufaransa, Italia na Uruguay.

Vijana wa Odera watakuwa na kibarua kigumu kushinda mchujo huo wa mataifa manne ikilinganishwa kuwa wanaorodheshwa katika nafasi hiyo ya chini kabisa katika orodha ya washiriki.

Hata hivyo, iwapo watafanikiwa kupata muujiza dhidi ya Amerika, Ureno na Hong Kong, basi watashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa tangu dimba hilo lianzishwe mwaka 1987.

Aidha, timu ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande almaarufu Shujaa itarejea mazoezini Septemba 27 kwa mashindano yanayokuja ya Safari Sevens na Raga za Dunia za msimu 2022-2023. Shujaa ya kocha Damian McGrath ilirudi nyumbani Septemba 12 kutoka Kombe la Dunia mjini Cape Town, Afrika Kusini.

Ilikamilisha dimba hilo la mataifa 24 katika nafasi ya 12 hapo Septemba 11.

  • Tags

You can share this post!

Ukraine yashtumu Urusi kwa kulenga kituo cha nyuklia

ZARAA: Matomoko ni yenye thamani kubwa kwake

T L