Habari Mseto

Roho mkononi waumini wakisubiri tangazo la Uhuru

June 6th, 2020 2 min read

Na VALENTINE OBARA

RAIS Uhuru Kenyatta anatarajiwa kutangaza mikakati mipya ya kuepusha ueneaji wa virusi vya corona leo, huku kukiwa na matarajio kuwa serikali italegeza baadhi ya kanuni zilizopo.

Jana, ripoti kuhusu mapendekezo ya kufungua shule na sehemu za kuabudu zilikabidhiwa kwa serikali kuu.

Waumini wengi na viongozi wa kidini wana matumaini serikali italegeza masharti kuhusu kufungwa kwa maeneo ya ibada kama vile makanisa na misikiti ambayo imekuwa ikifanya ibada kupitia mitandao na runinga.

Ilidhihirika kuwa shule zitaendelea kufungwa kwa muda usiojulikana.

Hayo yamejiri wakati ambapo idadi ya watu walioambukizwa virusi vya corona nchini ikiongezeka jana hadi 2,474 baada ya maambukizi 134 mapya kutangazwa jana.

Waziri Msaidizi wa Afya, Dkt Mercy Mwangangi alisema wengine 51 walipona, na kufikisha idadi ya waliopona hadi 643.

Idadi ya waliofariki ilifika 79 baada ya mtu mmoja kufa.

Ripoti ya jopo lililokusanya maoni kuhusu maeneo ya ibada ilikabidhiwa kwa Waziri wa Usalama wa Nchi, Dkt Fred Matiang’i, nayo ya masuala ya elimu ikakabidhiwa Prof George Magoha aliye Waziri wa Elimu.

Wawili hao walisema yaliyomo kwenye ripoti hizo yatatangazwa na Rais Kenyatta wakati wowote kuanzia leo.

Prof Magoha alibainisha kwamba itakuwa vigumu kuanza kufungua shule kwa sasa kwani shule nyingi zinatumiwa kama vituo vya karantini, zikiwemo taasisi za elimu ya juu.

“Shule 531 ni vituo vya karantini. Wizara itafanya tathmini ya ripoti hii kabla ya uamuzi wa mwisho kutolewa,” akasema.

Kwa upande mwingine, Dkt Matiang’i alisema serikali itaendelea kushauriana na viongozi wa kidini.

“Kazi yetu ilikuwa ni kuandaa ripoti. Yaliyomo kwenye ripoti yatatangazwa na Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa ya Usalama ambaye ni Rais wetu wakati ufaao,” akasema.

Katika Kaunti ya Mombasa, Kamishna Gilbert Kitiyo alisema kamati maalumu ya kaunti hiyo tayari imeorodhesha kanuni ambazo zitafaa kufuatwa na maeneo ya ibada endapo serikali kuu itaamua yafunguliwe.

Kanuni hizo za kaunti zitatumiwa sambamba na zile ambazo huenda zikatangazwa na serikali kuu.

Kulingana na Bw Kitiyo, zinajumuisha watu kukaa mbali na wenzao, kutumia vieuzi na kila mmoja kupimwa joto mwilini kabla kuingia katika sehemu ya ibada.

Aliongeza kuwa, maafisa wa serikali kuu kwa ushirikiano na wale wa kaunti watakagua kila sehemu kabla iruhusiwe kufunguliwa.