HabariSiasa

Roho ya Okoth yataabika

August 2nd, 2019 2 min read

Na BENSON MATHEKA

ROHO ya aliyekuwa mbunge wa Kibra, Ken Okoth, inaendelea kuhangaika wiki moja baada ya kifo chake, kufuatia mizozo kuhusu kupumzishwa kwa mwili wake.

Mizozo hiyo inahusu iwapo mwili wake utazikwa ama kuchomwa kama alivyotaka kabla ya kuaga dunia, atazikwa wapi na madai kwamba alikuwa na mke pembeni.

Jana, Mahakama Kuu ilipiga breki safari ya mwisho ya mbunge huyo kufuatia ombi la mwanamke anayedai kwamba alikuwa amezaa mtoto wa kiume na mbunge huyo.

Agizo la korti lilitolewa wakati ibada kwa heshima yake ilipokuwa ikiendelea katika shule ya upili ya wasichana ya Moi Girls katika eneobunge la Kibra, ambayo ilihudhuriwa na wanasiasa wa mirengo yote ya kisiasa.

Kwenye ombi lake, Ann Muthoni Thumbi, ambaye ni diwani wa kuteuliwa katika Kaunti ya Nairobi, anadai kwamba alizaa mtoto na Bw Okoth na hivyo anafaa kutambuliwa kama baba halisi ya mtoto wake kabla ya kuzikwa ama kuchomwa.

Bi Muthoni anadai kwamba mwili wa Bw Okoth ukichomwa itakuwa vigumu kufanyiwa uchunguzi wa DNA kuthibitisha ndiye baba ya mtoto wake.

Ametaja mama ya Okoth, Anjeline Ajwang, mkewe Monicah Okoth na mochari ya Lee kama washtakiwa katika ombi lake.

Ibada ya wafu ya kumuaga Bw Ken Okoth iliyofanyika katika Shule ya Upili Starehe Boys Centre, iliyofanyika Julai 31, 2019. PICHA | SILA KIPLAGAT

Agizo hilo linamaanisha kuwa mwili wa mbunge huyo aliyekufa Ijumaa iliyopita kutokana na kansa, hauwezi kuchomwa au kuzikwa hadi kesi hiyo isikilizwe na kuamuliwa.

Kabla ya mwanamke huyo kujitokeza, mamake marehemu Okoth alikuwa ametangaza kuwa mwanawe hakuwa amezaa mtoto na mwanamke yeyote ulimwenguni.

Wakati wa uhai wake, wengi walifahamu kwamba Bw Okoth alikuwa na mke mmoja, Monicah, ambaye alisema jana kuwa alimjua Bw Okoth kwa miaka 21 hadi kifo chake.

Monicah ametofautiana na mama ya Bw Okoth na wazee wa jamii ya Waluo wanaotaka mwili wake usichomwe alivyotaka mbunge huyo. Kulingana na Monicah na ndugu mdogo wa Bw Okoth, mapenzi ya mbunge huyo yalikuwa mwili wake uchomwe na wanataka yaheshimiwe.

Hata hivyo, mama yake na kaka ya marehemu wanasema mwili wa mwanawe unafaa kuzikwa katika boma lililoko kijiji cha Kasewe, eneobunge la Kabondo Kasipul, Kaunti ya Homa Bay.

Na hata Monicah akikubali mwili wa mumewe usichomwe, roho ya Bw Okoth haingetulia kwani kuna mvutano mwingine ambapo familia ya upande wa baba yake inataka azikwe kando ya kaburi la baba yake katika kijiji cha Kochia, Kaunti ya Homa Bay.

Ibada ya wafu ya kumuaga Bw Ken Okoth iliyofanyika katika Shule ya Upili ya Moi Girls, Kibra iliyofanyika Agosti 1, 2019. PICHA | SILA KIPLAGAT

Wazee wa upande wa babake wanakubaliana na mamake kwamba mwili wa mwanao haufai kuchomwa lakini wanatofautiana kuhusu unapofaa kuzikwa.

Kulingana na Baraza la Wazee wa jamii ya Waluo kupitia Mzee Nyandiko Ongadi, ni sharti mwili wa mbunge huyo uzikwe kwa kuzingatia desturi za jamii ya Waluo.

“Desturi za jamii yetu zinasema wake wa wana wetu wanafaa kukumbatia desturi za jamii ya Waluo,” alisema na kuongeza kuwa Monicah anafaa kuziheshimu tamaduni hizo.

Familia ya baba ya Bw Okoth inasema mama yake alikuwa ameolewa na Nicholas Anayo Obonyo, na kwa sababu alilipa mahari kabla ya kutengana na Anjeline, marehemu anatambuliwa kama mwana wao na hivyo anafaa kuzikwa kando ya kaburi la baba yake.

Msemaji wa familia hiyo, Raymond Mbai alimtaka Bi Anjeline kuheshimu desturi za jamii ya Waluo na kuruhusu mwili wa mwanawe kuzikwa Kochia.