Michezo

Roketi ya Victor Wanyama katika tuzo ya bao bora

January 1st, 2020 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

HUKU Victor Wanyama akizidi kuhusishwa na tetesi za kuondoka klabu yake ya Tottenham Hotspur katika kipindi kifupi cha uhamisho kinachoanza hii leo Jumatano, roketi ya nahodha huyo wa timu ya taifa ya Kenya dhidi ya Liverpool msimu uliopita inawania bao la mwongo.

Katika tovuti ya klabu hiyo ya jijini London, Uingereza, bao hilo la Wanyama limetiwa kwenye orodha ya mabao 25 yaliyofungwa kati ya mwaka 2010 na 2019 yanayowania tuzo hiyo.

Wanyama, ambaye tetesi zimekuwa zikisema anamezewa mate na Hertha Berlin (Ujerumani), Celtic (Scotland) na klabu za Uchina, aliingia mechi ya Liverpool kama mchezaji wa akiba zikisalia dakika 10 mchuano huo utamatike mnamo Februari 4, 2018.

Dakika mbili tu baada ya kujaza nafasi ya Mbelgiji Mousa Dembele, Wanyama alivuta kiki nzito kutoka nje ya kisanduku akaibwaga wavuni, na kufanya mabao kuwa 1-1 katika mechi hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Wanyama alianzisha shambulio hilo pembeni kushoto kabla ya mchezaji mwenza Christian Eriksen kupiga krosi ndani ya kisanduku.

Kipa Loris Karius alipangua mpira huo lakini ukaelekea upande wa Wanyama.

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 alikuwa anawasili karibu na kisanduku cha Liverpool kusaidia timu yake kutafuta bao la kusawazisha, alipokutana na mpira huo.

Alipiga shuti kali kutoka mita 27 ambalo Karius aliona likiwa ndani ya nyavu.

Bao hilo la Wanyama lilisaidia Tottenham kupata alama moja katika sare hiyo ya 2-2 dhidi ya Liverpool uwanjani Anfield.

Mmisri Mohamed Salah alifungia Liverpool dakika ya tatu na tena 91, huku Mwingereza Harry Kane akipachika penalti ya Spurs sekunde chache kabla ya mechi kumalizika, baada ya kupoteza penalti nyingine muda wa kawaida ukikaribia kukamilika.

Bao la mwongo

Goli la Wanyama, ambalo liliibuka goli la mwezi wa Februari 2018 la Tottenham, linawania bao la mwongo na yale ya Kane ya mwaka 2015 na 2016 dhidi ya Arsenal.

Pia itamenyanya na mabao ya Son Heung-min dhidi ya Crystal Palace, West Ham, Chelsea na Burnley kati ya mwaka 2017 na 2019; na goli la Emmanuel Adebayor dhidi ya Chelsea mwaka 2013.

Mabao ya Gareth Bale dhidi ya Stoke na Inter Milan (2010) na West Ham na Sunderland (2013), na Luka Modric dhidi ya Liverpool (2011) na Bolton (2013) pia yako katika orodha hiyo.

Orodha pia inajumuisha magoli mengine ya wachezaji Danny Rose, Peter Crouch, Kyle Walker, Gylfi Sigurdsson, Sandro, Christian Eriksen, Erik Lamela, Dele Alli na Lucas Moura.