Ronaldo afikia rekodi ya Rooney ya kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwezi katika EPL mara tano akivalia jezi za Man-United

Ronaldo afikia rekodi ya Rooney ya kutawazwa Mchezaji Bora wa Mwezi katika EPL mara tano akivalia jezi za Man-United

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo ametawazwa Mchezaji Bora wa Septemba 2021 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Nyota huyo raia wa Ureno aliyerejea uwanjani Old Trafford baada ya kuagana na Juventus ya Italia mnamo Agosti 2021 ameshinda tuzo hiyo kwa mara ya kwanza baada ya miaka 13.

Ronaldo aliibuka mshindi wa tuzo hiyo kwa mara ya tano akiwa mchezaji wa Manchester United baada ya kufunga mabao matatu ligini mnamo Septemba.

Ronaldo alipiku Allan Saint-Maximin, Joao Cancelo, Antonio Rudiger, Ismaila Sarr na Mohamed Salah waliokuwa pia wakiwania tuzo hiyo.

Akitumia mtandao wake wa Twitter, Ronaldo alisema: “Tija na fahari tele kuibuka mshindi wa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mwezi kati ya wanasoka wa haiba kubwa katika EPL”.

Mara ya mwisho kwa Ronaldo kuibuka Mchezaji Bora wa Mwezi katika EPL ni Machi 2008 baada ya kupachika wavuni mabao matano ligini chini ya kipindi cha wiki nne.

Miezi miwili kabla ya hapo, alitawazwa mshindi wa tuzo hiyo mnamo Januari 2008 na akaongoza Man-United kutia kapuni ubingwa wa EPL na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula huo.

Mataji yake mawili ya Mchezaji Bora wa Mwezi katika EPL yalipatikana kwa kipindi cha miezi miwili mfululizo mnamo Novemba na Disemba 2006.

Kwa kutawazwa Mchezaji Bora wa Septemba katika EPL, Ronaldo anafikia rekodi ya aliyekuwa fowadi wa Man-United, Wayne Rooney aliyewahi pia kunyanyua taji hilo mara tano.

Mabao yaliyoshindia Ronaldo tuzo hiyo mnamo Septemba ni mabao mawili aliyofunga katika ushindi wa 4-1 dhidi ya Newcastle United na goli jingine katika ushindi wa 2-1 dhidi ya West Ham United.

Ronaldo atapokezwa taji hilo pindi baada ya kurejea katika uwanja wa mazoezi wa Man-United, Carrington, baada ya Ureno kukamilisha mechi za kimataifa kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

MUTUA: Mwafrika amejihini na kujitweza mwenyewe

Mozzart yapiga jeki Harambee Stars kwa Sh3 milioni kucheza...