Michezo

Ronaldo afikisha mabao 101 ya kimataifa na kuweka rekodi mpya ya ufungaji katika timu ya taifa ya Ureno

September 9th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

CRISTIANO Ronaldo, 35, aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka wa kwanza kutoka bara Ulaya kuwahi kupachika wavuni mabao zaidi ya 100 ya kimataifa katika kabumbu ya wanaume.

Hii ni baada ya kufungia Ureno mabao mawili katika ushindi wa 2-0 dhidi ya Uswidi kwenye gozi la UEFA Nations League mnamo Septemba 8, 2020.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Ureno alifunga bao la kwanza katika dakika ya 45 kupitia mpira wa ikabu na kufikia rekodi ya magoli 100.

Ronaldo, ambaye kwa sasa ni fowadi wa Juventus nchini Italia, alipachika wavuni bao lake la 101 kunako dakika ya 72 ambalo lilikuwa la pili kwa upande wa Ureno.

Kwa sasa anasalia na mabao manane pekee ili kufikia rekodi ya dunia.

Ali Daei wa Iran ndiye mwanasoka wa pekee wa kiume anayejivunia idadi kubwa zaidi ya mabao kuliko Ronaldo. Katika enzi zake za usogora, Daei alipachika wavuni jumla ya mabao 109 kati ya mwaka wa 1993 na 2006.

Mgongo wa Ronaldo kwa sasa unasomwa na Sunil Chhtri wa India aliyewahi kufuma wavuni jumla ya mabao 72 na Lionel Messi ambaye amefungia Argnetina jumla ya magoli 70 hadi kufikia sasa.

Ushindi uliosajiliwa na Ureno dhidi ya Uswidi mnamo Septemba 8, 2020, ulikuwa wa pili kwa mabingwa hao watetezi wa Nations League kusajili katika kivumbi hicho cha mwaka huu.

Kibarua cha Ureno kilirahisishwa zaidi baada ya Gustav Svensson wa Uswidi kuonyeshwa kadi nyekundu mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kulishwa kadi mbili za manjano.

Hata hivyo, raha ya ushindi wa Ureno uliyeyushwa mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya nyota Bernardo Silva wa Manchester City kuondolewa uwanjani kwa machela kutokana na jeraha baya la msuli wa mguu.

Ureno wangalifunga idadi kubwa zaidi ya mabao katika mechi hiyo iwapo Bruno Fernandes aliyeshuhudia kombora lake likigongwa mwamba wa goli la Uswidi, angalitumia vizuri nafasi nyingi za wazi alizozipata.

Mechi hiyo ilikuwa ya 165 kwa Ronaldo aliyemfanyiza kipa Robin Olsen kazi ya ziada, kuchezea Ureno.

Takriban mabao 50 ya Ronaldo katika mechi za kimataifa yametokana baada ya kufikia umri wa miaka 30. Sogora huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid, amepachika wavuni jumla ya mabao 49 kutokana na michuano 47 ambayo ameshiriki akivalia jezi za Ureno tangu atimu umri wa miaka 30 mnamo 2015.