Michezo

Ronaldo afunga penalti na kusaidia Juventus kunyoa Lecce bila maji

June 27th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

CRISTIANO Ronaldo alipachika wavuni bao lake la 23 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu mnamo Juni 26, 2020, na kusaidia waajiri wake Juventus kupepeta Lecce 4-0 na hivyo kufungua pengo la alama saba zaidi kileleni mwa jedwali.

Lecce, waliokuwa wageni wa Juventus walijipata wakisalia na wachezaji 10 pekee uwanjani kunako dakika ya 31 baada ya beki Fabio Lucioni kuonyeshwa kadi nyekundu kwa kosa la kumkabili visivyo Ronaldo.

Fowadi mzawa a Argentina, Paulo Dybala aliwafungulia Juventus ukurasa wa mabao kunako dakika ya 53 kabla ya Ronaldo kufunga la pili kupitia mkwaju wa penalti katika dakika ya 62. Penalti hiyo ilikuwa zao la Ronaldo kuchezewa visivyo ndani ya kijisanduku cha Lecce.

Goli la tatu la Juventus lilifumwa wavuni na mshambuliaji Gonzalo Higuain, 32, aliyeshirikiana vilivyo na Ronaldo katika dakika ya 83, sekunde chache kabla ya beki Matthijs de Ligt kukizamisha kabisa chombo cha wageni wao.

Ronaldo, ambaye pia alifunga penalti katika ushindi wa 2-0 uliosajiliwa na Juventus dhidi ya Bologna mnamo Juni 22, 2020, sasa anajivunia kufunga jumla ya mabao 23 kutokana na mechi 24 za hadi kufikia sasa msimu huu.

Juventus kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Serie A kwa alama 69, saba zaidi kuliko nambari mbili Lazio. Lecce wananing’inia padogo mkiani mwa jedwali kwa alama 25 na wapo katika hatari ya kushushwa ngazi kwa pamoja na Spal na Brescia.