Ronaldo afungia Juventus mabao mawili dhidi ya Udinese na kutua kileleni mwa orodha ya wafumaji bora Serie A

Ronaldo afungia Juventus mabao mawili dhidi ya Udinese na kutua kileleni mwa orodha ya wafumaji bora Serie A

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga mabao mawili na kuchangia moja jingine katika ushindi wa 4-1 ulioandikishwa na Juventus dhidi ya Udinese katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Jumapili.

Ronaldo aliwafungulia Juventus ukurasa wa mabao kupitia krosi ya Aaron Ramsey katika dakika ya 31 kabla ya kuchangia goli la pili lililopachikwa wavuni na Federico Chiesa katika dakika ya 49.

Ronaldo kwa sasa anajivunia mabao 14 kutokana na mechi 11 zilizopita za Serie A, ufanisi ambao unamweka kileleni ma orodha ya wafungaji bora wa Serie A msimu huu.

Marvin Zeegelaar alifuma bao lililofuta machozi ya Udinese katika dakika ya 90, sekunde chache kabla ya Paulo Dybala kuongeza goli la nne kwa upande wa Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa taji la Serie A.

Chini ya kocha Andrea Pirlo, Juventus kwa sasa wanashikilia nafasi ya tano kwa alama 27 japo pengo la pointi 10 linatamalaki kati yao na viongozi AC Milan ambao wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko Juventus.

Kichapo ambacho Udinese walipokezwa kiliwateremsha hadi nafasi ya 13 kwa alama 15 sawa na Fiorentina. Udinese kwa sasa hawajasajili ushindi wowote katika msururu wa michuano minne iliyopita.

You can share this post!

Barcelona waponea dhidi ya Huesca katika Ligi Kuu ya...

Masharti makali shuleni