Michezo

Ronaldo afungia Juventus mabao mawili na kufikia rekodi ya Lewandowski barani Ulaya

December 20th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alipachika wavuni mabao mawili na kusaidia Juventus kudumisha rekodi ya kutopigwa hadi kufikia sasa kwenye kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) baada ya kupepeta Parma 4-0 uwanjani Ennio-Tardin mnamo Jumamosi.

Fowadi chipukizi raia wa Uswidi, Dejan Kulusevski, 20, alifungulia Juventus ukurasa wa mabao katika dakika ya 23 baada ya kushirikiana pakubwa na Alex Sandro.

Ronaldo alipachika wavuni goli la pili la Juventus dakika tatu baadaye kabla ya kufunga lake la 12 hadi kufikia sasa ligini mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Alvaro Morata alizamisha kabisa chombo cha Parma mwishoni mwa kipindi cha pili kwa kufunga bao la nne la Juventus kupitia krosi aliyopokezwa na Federico Bernardeschi.

Chini ya kocha Andrea Pirlo, Juventus kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Serie A licha ya kusajili sare mara sita kutokana na jumla ya michuano 13 iliyopita ligini.

Fowadi wa Juventus Mreno Cristiano Ronaldo (kati) baada ya kufunga bao lake la pili wakati Parma na  Juventus zilikabiliana katika Serie A uwanjani Ennio-Tardini mjini Parma, Desemba 19, 2020, na wageni wakavuna ushindi wa 4-0. Picha/ AFP

Ushindi dhidi ya Parma unatarajiwa kuwawekea presha viongozi wa jedwali AC Milan ambao kwa sasa wamejizolea alama 28 kutokana na mechi 12 zilizopita.

Mbali na Milan, Juventus ambao ni mabingwa mara tisa wa taji la Serie A ndizo klabu za pekee ambazo hazijashindwa ligini miongoni mwa vikosi vya Ligi Kuu tano za bara Ulaya hadi kufikia sasa msimu huu.

Ronaldo ambaye alipoteza penalti katika sare ya 1-1 iliyosajiliwa na Juventus dhidi ya Atalanta mnamo Disemba 18, kwa sasa anajivunia mabao 63 kutokana na mechi 73 ambazo amesakata kwenye kampeni za Serie A.

Kwa pamoja na Robert Lewandowski wa Bayern Munich, Ronaldo, 35, ambaye pia amewahi kuchezea Manchester United na Real Madrid, anashikilia rekodi ya ufungaji bora miongoni mwa vikosi vya Ligi Kuu tano za bara Ulaya hadi sasa mwaka huu wa 2020. Wawili hao wana mabao 32 kila mmoja.