Ronaldo afungia Juventus mawili na kuendeleza masaibu ya Crotone mkiani mwa jedwali la Serie A

Ronaldo afungia Juventus mawili na kuendeleza masaibu ya Crotone mkiani mwa jedwali la Serie A

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga mabao mawili kupitia kichwa na kusaidia Juventus kunyanyasa Crotone wanaovuta mkia wa jedwali la Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Jumatatu usiku.

Ushindi wa 3-0 uliosajiliwa na Juventus katika mchuano huo uliwapaisha hadi nafasi ya tatu kwa alama 45, nane pekee nyuma ya viongozi Inter Milan ambao wamesakata mchuano mmoja zaidi kuliko masogora hao wa kocha Andrea Pirlo.

Ronaldo alifuma wavuni goli la kwanza katika dakika ya 38 kutokana na krosi ya Alex Sandro kabla ya kukamilisha tena kwa kichwa pasi ya hewani aliyomegewa na kiungo wa zamani wa Arsenal, Aaron Ramsey mwishoni mwa kipindi cha kwanza.

Magoli hayo ya mawili yalifikisha idadi ya mabao ya Ronaldo katika soka ya Serie A hadi 70 chini ya kipindi cha miaka miwili na nusu iliyopita.

Crotone inakuwa timu ya 78 inayoshiriki mojawapo ya Ligi Kuu tano za soka ya bara Ulaya kufungwa na Ronaldo – nyota raia wa Ureno ambaye pia amewahi kuchezea Manchester United na Real Madrid.

Bao la tatu la Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa Serie A, lilipachikwa wavuni na Weston McKennie katika dakika ya 66.

Ronaldo kwa sasa ndiye anayeongoza orodha ya wafungaji bora katika Serie A. Anajivunia magoli 18, moja zaidi kuliko nambari mbili Romelu Lukaku anayetiwa makali na kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte kambini mwa Inter.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

BI TAIFA FEBRUARI 23, 2021

Crystal Palace wazamisha chombo cha Brighton na kumweka...