Michezo

Ronaldo aibeba Juventus kupiga Sassuolo

September 17th, 2018 1 min read

MSHAMBULIZI  wa Ureno Cristiano Ronaldo Jumapili alifungua rasmi akaunti yake ya magoli kwa klabu yake mpya ya Juventus wakati wa mechi kati ya mabingwa hao watetezi wa ligi ya Serie A na Sassuolo.

Ronaldo ambaye awali alisakatia Sporting Lisbon, Manchester United na Real Madrid alifunga mabao mawili katika ushindi huo wa 2-1 na kuendeleza mwanzo nzuri wa mibabe hao wa soka ya Italia ambao wametwaa ushindi katika mechi zote nne za mwanzo wa msimu wa 2018/19.

Mwanadimba huyo aliye na umri wa miaka 33 alimimina wavuni bao la kwanza dakika ya 47 punde tu baada kipindi cha pili kung’oa nanga kisha akaongeza la pili dakika 60 ya mechi. Bao la kufuta machozi la Sassuolo lilitiwa wavuni na mchezaji Khouma Babacar katika dakika ya 90.

Ingawa Ronaldo hakuwa amebusu nyavu za wapinzani katika mechi tatu zilizopita tangu kusajiliwa kwake, mkufunzi wake Massimiliano Allegri  alieleza kutotaabishwa na hilo haswa ikizingatiwa mwanadimba huyo alikuwa amelenga shuti 23 langoni katika mechi hizo.

“Sikutarajia Ronaldo ajitume zaidi kuliko jinsi  alivyokuwa katika mechi tatu zilizopita kwa sababu ilikuwa ni muda tu kisha aanze kufunga,” akasema Allegri.

Straika huyo alifunga mabao 44 kwa Real Madrid msimu wa 2016/17.  Kati ya mabao yote, 15 aliyoyafunga katika michuano ya ligi ya Bara Uropa yalisaidia Real kutwaa ubingwa wa ligi hiyo kwa mwaka wa tatu mfululizo.