Michezo

Ronaldo aongoza Juventus kuzamisha Genoa, anusia rekodi mpya ya ufungaji katika soka ya Italia

July 1st, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

CRISTIANO Ronaldo alifunga bao na kuwasaidia Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) kuwabamiza Genoa 3-1 mnamo Juni 30, 2020.

Matokeo hayo yaliwezesha Juventus ya kocha Maurizio Sarri kudumisha pengo la alama nne kati ya na nambari mbili Lazio kileleni mwa jedwali.

Baada ya kutoshana nguvu na wenyeji wao katika kipindi cha kwanza, Juventus walifungiwa ukurasa wa mabao kupitia kwa Paulo Dybala katika dakika ya 50 kabla ya Ronaldo kufunga goli lake la 24 hadi kufikia sasa msimu huu kutokea hatua ya 25.

Douglas Costa aliwafungia Juventus bao la tatu kunako dakika ya 73 kabla ya Andrea Pinamonti kuwafutia Genoa machozi mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ronaldo kwa sasa anajivunia jumla ya mabao 726 katika taaluma yake ya usogora katika ngazi ya klabu na timu ya taifa.

Mshindani wake mkuu katika ulingo wa sasa wa soka, Lionel Messi anajivunia jumla ya mabao 700.

Ronaldo kwa sasa anasalia na bao moja pekee kabla ya kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Juventus baada ya Omar Sivori mnamo 1960-61 kuwahi kufunga mabao 25 katika msimu mmoja wa Serie A.

Juventus kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Serie A kwa alama 72, nne zaidi kuliko Lazio waliowacharaza Torino 2-1 katika mchuano mwingine wa Juni 30, 2020.