Michezo

Ronaldo arejea ugani kwa matao ya juu baada ya kupona Covid-19

November 2nd, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alitokea benchi na kufunga mabao mawili yaliyosaidia Juventus kupepeta Spezia 4-1 katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A).

Mechi hiyo ilikuwa ya kwanza kwa Ronaldo kusakata tangu kuugua Covid-19 na kusalia nje ya kikosi cha Juventus kwa kipindi cha majuma mawili.

Baada ya kuugua, nyota huyo mwenye umri wa miaka 35 alikosa mechi nne zilizotandazwa na waajiri wake. Baada ya kuingizwa uwanjani dhidi ya Spezia, Ronaldo alifanya mambo kuwa 2-1 baada ya dakika tatu pekee kabla ya kufunga penalti. Adrien Rabiot ndiye aliyefunga bao la tatu la Juventus baada ya Alvaro Morata kufungua ukurasa wa magoli.

Spezia ambao ni limbukeni wa Ligi Kuu ya Serie A, walifutiwa machozi na fowadi Tommaso Pobega. Ushindi kwa Juventus uliwapaisha hadi nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali kwa alama 12, nne nyuma ya viongozi AC Milan.

Ronaldo aliugua corona mnamo Oktoba 13 na akakosa mechi ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) iliyoshuhudia Juventus wakipokezwa kichapo cha 2-0 na Barcelona jijini Turin mnamo Oktoba 28, 2020. Hiyo ilikuwa baada ya Ronaldo kupatikana na virusi vya corona kwa mara ya pili mnamo Oktoba 27.

Wakati akiugua, Ronaldo alikosa pia mechi mbili za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) na michuano miwili iliyosakatwa na waajiri wake kwenye UEFA. Hadi alipochezeshwa dhidi ya Spezia, mara ya mwisho kwa Ronaldo kuwajibishwa ugani ni katika gozi la UEFA Nations League lililokutanisha Ureno na Ufaransa mnamo Oktoba 11, 2020.

Hadi alipougua corona, Ronaldo alikuwa amefungia Juventus mabao matatu kutokana na mechi mbili za ufunguzi wa kampeni za msimu huu wa 2020-21.

Mechi kati ya UEFA Juventus na Barcelona ilitazamiwa kutoa jukwaa kwa Ronaldo na Lionel Messi kukutana kwa mara ya kwanza baada ya miaka miwili. Nyota hao wawili ndio wanasoka bora zaidi duniani kwa sasa huku wakijivunia kutwaa mataji 11 ya Ballon d’Or – Messi mara sita na Ronaldo mara tano.

Huenda fursa hiyo kwa sasa ikawa kwenye marudiano ya mkondo wa pili katika mechi ya makundi ya UEFA mnamo Disemba 8, 2020 uwanjani Camp Nou.