Ronaldo atakuwa tegemeo letu dhidi ya FC Porto – Juventus

Ronaldo atakuwa tegemeo letu dhidi ya FC Porto – Juventus

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo, 36, anatarajiwa kuongoza leo kampeni za Juventus watakaoalika Porto FC ya Ureno katika marudiano ya hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Juventus ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A), watashuka dimbani wakiwa na kibarua kigumu cha kubatilisha kichapo cha 2-1 walichopokezwa na Porto katika mchuano wa mkondo wa kwanza jijini Lisbon, Ureno mnamo Februari 17, 2021.

Ronaldo ambaye pia amewahi kuchezea Sporting CP, Manchester United na Real Madrid, alisazwa benchi kwa dakika 60 wakati wa mechi ya Serie A iliyowakutanisha Juventus na Lazio mnamo Machi 6, 2021. Juventus ya kocha Andrea Pirlo ilisajili ushindi wa 3-1 katika gozi hilo.

“Ana hamu ya kutufungia mabao muhimu yatakayotuwezesha kusonga mbele katika kivumbi cha UEFA muhula huu. Alipumzika vya kutosha wikendi iliyopita na tuna matarajio makuu kutoka kwake,” akasema Pirlo kuhusu Ronaldo ambaye ni mshindi mara tano wa taji la UEFA.

“Tunajua presha iliyopo mbele, hasa kutoka kwa mashabiki wetu. Hata hivyo, naamini tuna kila sababu ya kubwaga Porto na kupiga hatua hadi robo-fainali. Tuna wanasoka matata wenye uwezo wa kuweka hai azma yetu hiyo,” akaongeza Pirlo aliyeaminiwa kuwa mrithi wa mkufunzi Maurizio Sarri mwishoni mwa kampeni za msimu wa 2019-20.

Juventus ambao kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la Serie A, walibanduliwa na Olympique Lyon kwenye hatua ya 16-bora ya UEFA mnamo 2019-20.

Mbali na Ronaldo, mwanasoka mwingine mzoefu atakayekuwa tegemeo la Juventus leo ni beki Giorgio Chiellini atakayeziba pengo la Matthijs de Ligt anayeuguza jeraha.

Porto watashuka dimbani wakilenga kufuzu kwa robo-fainali za UEFA kwa mara ya pili chini ya kipindi cha misimu mitatu iliyopita.

Licha ya makali yao kushuka msimu huu, Juventus wamefungwa magoli sita pekee kutokana na mechi 13 zilizopita katika mashindano yote. Aidha, wameshinda jumla ya mechi saba zilizopita katika uwanja wao wa nyumbani na kufunga angalau mabao mawili katika kila mojawapo.

Uthabiti wa Juventus katika uga wa Allianz Stadium jijini Turin, umeshuhudia masogora hao wa Pirlo wakishinda mechi 10 na kuambulia sare mara mbili kutokana na jumla ya michuano 13 iliyopita ya Serie A. Matokeo hayo yanawadumisha sasa katika nafasi ya tatu jedwalini kwa alama 52, saba nyuma ya viongozi Inter Milan.

Nafuu zaidi kwa Juventus wanaofukuzia taji la Serie A kwa msimu wa 10 mfululizo, ni kwamba wana mchuano mmoja zaidi wa kutandaza ili kufikia idadi ya mechi ambazo zimesakatwa na washindani wakuu – Inter na AC Milan wanaokamata nafasi ya pili jedwalini kwa pointi 56.

Kwa kushinda Juventus katika mkondo wa kwanza, Porto waliendeleza rekodi ya kutopigwa kwenye gozi la UEFA katika jumla ya mechi sita mfululizo. Hii ni mara ya 24 kwa wapambe hao wa soka ya Ureno kunogesha kipute cha UEFA. Ni Real Madrid na Barcelona pekee kutoka Uhispania ambao wameshiriki kivumbi hicho mara nyingi zaidi (mara 25 kila mmoja).

Chini ya mkufunzi Sergio Conceicao, Porto kwa sasa wanashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Ureno (Primeira Liga) kwa alama 48 huku pengo la pointi 10 likitamalaki kati yao na viongozi Sporting CP.

Kikosi hicho kilikomesha ukiritimba wa Benfica kwenye soka ya Primeira Liga mnamo 2019-20 na kutwaa ubingwa kwa mara ya 29. Porto wataingia katika mechi ya leo wakijivunia motisha ya kupiga Gil Vicente 2-0 katika mechi yao iliyopita ligini.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Inter Milan wapiga Atalanta na kufungua pengo la alama sita...

Nafuu Dortmund baada ya Haaland kupona kabla ya mechi dhidi...