Ronaldo avunja rekodi ya ufungaji wa mabao kwenye soka ya Euro kwa wanaume

Ronaldo avunja rekodi ya ufungaji wa mabao kwenye soka ya Euro kwa wanaume

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo aliweka rekodi ya kuwa mfungaji bora wa soka ya wanaume kwenye kampeni za Euro baada ya kufunga mabao mawili mnamo Jumanne na kusaidia Ureno kupepeta Hungary 3-0 katika mchuano wa ufunguzi wa kampeni za Kundi F.

Ronaldo ambaye ni fowadi matata wa Juventus, alifungia Ureno bao la pili katika dakika ya 87 kupitia penalti baada ya Raphael Guerreiro kufungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 84. Penalti hiyo ya Ureno ilisababishwa na tukio la Rafa Silva kuchezewa visivyo na beki Willi Orban ndani ya kijisanduku.

Bao la Ronaldo lilikuwa lake la 10 kwenye kampeni za Euro, na hivyo akavunja rekodi ya awali ya magoli tisa iliyokuwa ikishikiliwa na mwanasoka wa zamani wa timu ya taifa ya Ufaransa, Michel Platini.

Ronaldo alipachika wavuni bao lake la 11 kwenye kivumbi cha Euro mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kumzidi maarifa kipa Peter Gulacsi wa Hungary.

Mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester United na Real Madrid ndiye mfungaji bora wa muda wote katika kikosi cha Ureno na anajivunia jumla ya mabao 105 kimataifa.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Yatani kutuma Sh39 bilioni kwa kaunti baada ya magavana...

Jumwa apuuza hitaji la digrii kwa uongozi wa kisiasa