Michezo

Ronaldo aweka rekodi Italia

July 21st, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

NYOTA Cristiano Ronaldo, 35, aliweka rekodi ya kuwa mwanasoka wa kwanza kuwahi kufunga mabao 50 akichezea ligi za Italia (Serie A), Uhispania (La Liga) na Uingereza (EPL) baada ya kufungia Juventus magoli mawili dhidi ya Lazio mnamo Julai 20, 2020.

Juventus kwa sasa wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Italia kwa alama 80, nane zaidi kuliko nambari mbili Inter Milan wanaotiwa makali na kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte.

Ushindi wa 2-1 uliosajiliwa na Juventus dhidi ya Lazio kwa sasa unawaweka katika uhitaji wa alama nne pekee kutokana na mechi nne zilizosalia ili kutia kapuni ubingwa wa taji la Serie A kwa mara ya tisa mfululizo. Taji litakalonyanyuliwa na Juventus msimu huu litakuwa la kwanza kwa kocha Maurizio Sarri kutia kapuni kwenye ligi katika historia yake ya ukufunzi.

Ronaldo aliwafungulia Juventus ukurasa wa mabao kunako dakika ya 51 kupitia penalti kabla ya kukamilisha krosi ya fowadi Paulo Dybala kwa ustadi mkubwa kunako dakika ya 54.

Ciro Immobile aliwafutia Lazio macho kupitia mkwaju wa penalti mwishoni mwa kipindi cha pili baada ya kuchezewa visivyo na beki Leonardo Bonucci. Matokeo hayo yaliwasaza Lazio katika nafasi ya nne kwa alama 69, mbili nyuma ya Atalanta wanaofunga mduara wa tatu-bora.

Ronaldo na Immobile kwa sasa wanashikilia nafasi ya kwanza kwenye orodha ya wafungaji bora wa Serie A hadi kufikia sasa msimu huu kwa mabao 30 kila mmoja. Ronaldo ambaye ni mzawa wa Ureno analenga kuweka rekodi ya kuwa mwanasoka wa kwanza wa Juventus baada ya Alessandro del Piero mnamo 2007-08 kuwahi kutawazwa kiatu cha dhahabu kwa kuibuka mfumaji bora wa Serie A.

REKODI YA RONALDO KATIKA LIGI ZA BARA ULAYA:

EPL: Mabao 84 kutokana na mechi 196 akichezea Man-United.

LA LIGA: Mabao 311 kutokana na mechi 292 akichezea Real Madrid.

SERIE A: Mabao 51 kutokana na mechi 61 akichezea Juventus.

Ronaldo ndiye mwanasoka wa tatu wa Juventus kuwahi kupachika wavuni mabao 30 katika msimu mmoja wa Serie A huku Immobile akiwa mwanasoka wa tano mzawa wa Italia kufikia kiwango hicho cha ufanisi.

Ronaldo na Immobile pia wamefikia rekodi ya 1995-96 ya Giuseppe Signori aliyewahi kufunga idadi kubwa zaidi ya penalti (mikwaju 12) katika soka ya Serie A.

Ronaldo ndiye mchezaji wa kwanza katika Serie A kuwahi kufunga mabao 50 haraka zaidi (kutokana na mechi 61 pekee). Bao lake la pili dhidi ya Lazio lilikuwa la 51 hadi kufikia sasa tangu aagane rasmi na Real Madrid ya Uhispania mnamo Julai 2018.