Michezo

Ronaldo azamisha chombo cha Barcelona kikiwa na nguli Messi

December 9th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga penalti mbili na kufikisha idadi yake ya mabao kwenye Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kuwa 134 mnamo Disemba 8, 2020.

Magoli hayo ya Ronaldo yalisaidia waajiri wake Juventus kupepeta Barcelona 3-0 katika mechi ya mwisho ya Kundi G. Ronaldo aliwaweka Juventus kifua mbele katika dakika ya 13 baada ya kuchezewa visivyo na beki raia wa Uruguay, Ronald Araujo.

Juventus walifungiwa bao la pili na Weston McKennie katika dakika ya 20 kabla ya Ronaldo kuzamisha chombo cha wenyeji wao kupitia penalti iliyosababishwa na beki Clemet Lenglet katika dakika ya 52.

“Hatukujituma vilivyo. Tulitepetea kuanzia mwanzo na tukazidiwa maarifa katika takriban kila idara. Juventus walicheza vizuri,” akasema kocha Ronald Koeman.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza tangu 2016 kwa Barcelona kupoteza katika hatua ya makundi ya UEFA.

Ni mchuano uliokutanisha Lionel Messi na Ronaldo ambao wanachukuliwa kuwa wachezaji bora zaidi kwa sasa duniani kwa mara ya kwanza uwanjani tangu Mei 2018.