Ronaldo na nduguze wanunulia mama yao zawadi ya benzi nyeusi

Ronaldo na nduguze wanunulia mama yao zawadi ya benzi nyeusi

Na CHRIS ADUNGO

DOLORES Aveiro alishindwa kuzuia furaha yake baada ya kupokezwa zawadi ya gari kutoka kwa mwanawe Cristiano Ronaldo na nduguze watatu.

Dolores mwenye umri wa miaka 65 alizawidiwa gari jeusi aina ya Mercedes Benz lenye thamani ya Sh36 milioni na shada la maua kutoka kwa wanawe wanne – Ronaldo, Elma, Katia na Hugo baada ya kuruhusiwa kuondoka hospitalini.

Mama huyo mwenye umri wa miaka 65 alikuwa amelazwa katika hospitali ya Funchal inayomilikiwa na Ronaldo mjini Funchal, Ureno kwa miezi mitatu iliyopita baada ya kuugua kiharusi.

“Asanteni sana wanangu kwa zawadi hizi za kutamanisha. Mmeonyesha ishara kubwa ya mapenzi. Nimepokea tuzo hizi kwa moyo mmoja. Mola awazidishie,” akaandika Dolores kwenye mtandao wake wa Instagram.

Dolores ambaye aliwapongeza wazazi wote wa kike duniani, alituzwa na wanawe siku ambapo Maadhimisho ya Siku ya Kina Mama Duniani yalikuwa yakifanywa nchini Ureno na Uhispania.

Katia ambaye ni bintiye Dolores anayeishi Brazil, alisema, “Unastahiki tuzo hizo mama. Unastahili kutuzwa hii dunia nzima iwe yako. Tupo hapa kwa ajili yako. Tunakujali sana ndiyo maana unasalia katika fikra zetu siku zote.”

Ronaldo ambaye amekuwa katika ziara ya kuponda raha jijini Madeira, Ureno tangu Machi 9, alionekana jana akiwa ameandamana na mchumba wake Georgina Rodriguez na mwanawe wa kwanza, Cristiano Jr.

Katika baadhi ya picha walizopigwa kwa pamoja katika eneo la Canical, Ureno, nyota huyo wa zamani wa Manchester United, aliandika “wapo wanawake wawili ninaowastahi zaidi duniani kwa pendo la kweli: Dolores na Georgina ambaye ni zawadi kuu kwangu kutoka kwa Mola wangu.”

Katika picha nyingine, Ronaldo alionekana akiwa amekumbatiwa na mamaye huku wote wakiwa wamevaliwa na tabasamu.

Picha nyinginezo zilimwonyesha Ronaldo akiwa usingizini huku Georgina akimpiga mabusu motomoto kwenye paji lake la uso.

Ronaldo anatazamiwa kurejea nchini Italia wiki hii kisha kujitenga akijifanyia mazoezi wakati akisubiri kuanza upya kwa kampeni za Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu.

Dolores amekuwa akiwataarifu mashabiki wake kuhusu maendeleo yake ya afya mara kwa mara kwa kutuma picha mitandaoni akiwa nyumbani tangu aliporuhusiwa kuondoka hospitalini.

Ronaldo ambaye amewahi pia kuchezea Real Madrid nchini Uhispania, amekuwa akiishi katika hoteli moja viungani mwa mji wa Canical akitozwa ada ya Sh490,000 kwa siku. Hoteli hiyo inapakana na jumba la kibiashara la ghorofa saba lililonunuliwa na Ronaldo mwaka jana.

You can share this post!

Gavana wa Kiambu awajali wagonjwa

Simbas watoa mwongozo mpya wa kuboresha raga nchini Kenya

adminleo