Michezo

Rooney afungia Derby frikiki kuzamisha Norwich

October 3rd, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

FRIKIKI ya dakika za mwisho kutoka kwa Wayne Rooney iliwapa Derby County ushindi wa 1-0 uliowavunia alama tatu za kwanza katika Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship).

Rooney alichanja mpira huo wa ikabu kutoka hatua ya 20 na kumwacha hoi kipa Tim Krul wa Norwich City dakika tatu kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa.

Norwich walisalia kujilaumu wenyewe katika mchuano huo ulioshuhudia fowadi Teemu Pukki akipoteza mkwaju wa penalti katika dakika ya 49 uwanjani Carrow Road.

Penalti iliyopaishwa na Pukki ilitokana na tukio la beki George Evans kunawa mpira alioelekezwa na kiungo Onel Hernandez.

Ingawa Norwich waliazimia kutumia vyema uwanja wao wa nyumbani, juhudi zao zilizimwa na kipa David Marshall aliyesalia imara katikati ya michuma ya goli la Derby.

Kocha Phillip Cocu wa Derby alikifanyia kikosi chake kilichopepetwa na Blackburn 4-0 mnamo Septemba 26, 2020 mabadiliko manne muhimu.

Mchuano huo ulikuwa wa tatu mfululizo kwa Derby kupoteza katika kampeni za Championship msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO