Makala

ROSE KYULE: Lupita amenipa motisha

April 26th, 2020 2 min read

Na JOHN KIMWERE

AMEPANIA kutinga upeo wa kimataifa kama mwigizaji wa kike maana anaamini anatosha mboga katika masuala ya maigizo. Pia anaorodheshwa kati ya wasanii wa kike ambao wamejifunga kimbwembwe kuvumisha tasnia ya uigizaji hapa nchini.

Binti huyu Rose Nduku Kyule anasema tayari ametizima azma ya kwanza hasa kuonekana kwenye runinga ambapo sasa analenga kufikia hadhi ya waigizaji maarufu Afrika.

Kisura huyu anasema tangu akiwa mtoto alitamani sana kuwa mtangazaji mtajika kwenye runinga. Kando na uigizaji binti huyu ni video vixen anayelenga kumiliki brandi ya kuzalisha filamu ili kukuza waigizaji wanaoibukia.

”Kiukweli nimepiga hatua katika uigizaji tangu mwaka 2016 nilipoanza kujituma katika masuala ya maigizo,” anasema na kuongeza kuwa alianza kushiriki filamu kwa kutumia mwogozo wa vitabu za riwaya (setbooks). Kipindi hicho alifanya kazi na vikundi viwili, Informatrix Productions na Hatua Theatre Production.

”Sina shaka kutaja kwamba nilipata motisha zaidi kushiriki filamu baada ya kutazama kazi ya msanii Neomi Ng’ang’a aliyekuwa anaigiza katika kipindi cha Sumu la penzi mwaka 2016/2017,” alisema na kuongeza kuwa kipindi hicho alikuwa mwanafunzi wa mwaka wa kwanza katika chuo cha Zetech alikokuwa akisoma kuhitimu kama mwana habari.

Lakini kwa sasa ndoto hiyo ilibakia stori tu kwa kuzingatia uigizaji ulimfanya aache shule.

Kama video vixen mwaka uliyopita alibahatika kushiriki nyimbo moja kwa jina Urembo ni bonus iliyotungwa na vijana barubaru. Binti huyu anajivunia kuingiza zaidi ya filamu sita ambazo zimefanikiwa kupata mpenyo na kupeperushwa kwenye runinga.

Mwanzo wa ngoma mwaka 2016 alishiriki filamu iitwayo Varshita chini ya Moonbeam Productions ambayo hupepersushwa kupitia Maisha Magic East.

Kisura huyu pia ameigiza filamu zingine ikiwamo: Auntie boss na Real househelps of Kawangware ambazo hupeperushwa kupitia runinga ya NTV inayomilikiwa na Nation Media Group. Pia ameigiza filamu ya Njoro wa Uba ambayo hupeperushwa kupitia Maisha Magic East.

Kyule anasema anatamani sana kufikia upeo wa mwigizaji mwenzake Mkenya, Lupita Nyong’o anayezidi kutesa kwenye filamu za Hollywood. Lupita alipata umaarufu alipoigiza filamu iitwayo 12 Years a slave.

”Bila mapendeleo Lupita ametutia motisha waigizaji wengi wanaokuja hapa nchini pia katika mataifa mengine duniani,” alisema na kuongeza kuwa baadhi yao wanatamani sana kufikia kiwango hicho.

Kwa waigizaji wa humu nchini, msichana huyu aliyezaliwa mwaka 1998 anasema angependa sana kufanya kazi nao Neomi Ng’ang’a (Sumu la Penzi) na Catherine Kamau Karanja(Plan B) na (Sue and Johny) kati ya zingine.

Kwa wasanii wa filamu za Kinigeria (Nollywood) anatamani sana kufanya kazi na waigizaji kama Eniola Badmus na Funke Akindele.

Eniola Badmus anajivunia kuigiza filamu kama ‘Jenifa,’ ‘Ghetto Bred,’ ‘The Return of Jenifa,’ ‘Black Val,’ ‘Divorce not allowed,’ na ‘Boss of all Bosses,’ kati ya zingine.

Kisura huyu anashukuru mamake mzazi, Janet Nthenya na mwigizaji Ben Tekee ambao wamekuwa mstari wa mbele kumshika mkono kwa mawaidha katika masuala ya maigizo.