Habari Mseto

Rotich arekebisha makosa katika ufadhili wa nyumba za wafanyakazi

June 21st, 2018 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Wananchi wanaofanya kazi katika sekta rasmi hawatatozwa asilimia moja kufadhili hazina ya maendeleo ya ujenzi wa nyumba kama ilivyopendekezwa katika Mswada wa Fedha 2018.

Ripoti hii ni kwa mujibu wa Waziri wa Fedha Bw Henry Rotich Jumanne. Hata hivyo, watatozwa asilimia 0.5.

Kulingana na waziri huyo, asilimia moja katika mswada huo ilikuwa ni makosa ya uandishi na yatarekebishwa.

“Makosa hayo yatarekebishwa mswada huo ukifikishwa Bungeni,” alisema Bw Rotich.

Kulingana na waziri huyo, Wizara ya Nyumba ilikuwa imependekeza asilimia tano, lakini Hazina ya Fedha ikapunguza hadi asilimia 0.5 kwa sababu asilimia iliyopendekezwa ilikuwa ya juu sana.

Ikiwa makosa hayo hayatarekebishwa, huenda wafanyikazi wakaumizwa zaidi na ada hiyo.

Ni wakati wa kwanza kwa Wizara ya Nyumba kutekeleza hazina hiyo licha ya kuwa katika sheria kuhusu nyumba kwa miaka mingi.