Michezo

Rotterdam Marathon, mbio alizosubiria kwa hamu kubwa Kiptum zatimkwa Uholanzi

April 14th, 2024 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa Eindhoven Marathon Kenneth Kipkemboi ni mmoja wa watimkaji wanaopigiwa upatu kutwaa taji la Rotterdam Marathon nchini Uholanzi, Jumapili.

Makala haya yatamkumbuka Kelvin Kiptum aliyeaga dunia mnamo Februari 11 katika ajali mbaya ya barabarani, siku chache baada ya rekodi yake ya dunia ya saa 2:00:35 kurasimishwa na Shirikisho la Riadha Duniani mnamo Februari 6.

Kiptum alikuwa ametangaza wazi nia yake ya kukamilisha mbio hizo za kilomita 42 chini ya saa mbili. Washiriki watanyamaza kwa dakika moja kwa heshima ya Kiptum.

Kipkemboi alikamata nafasi ya tisa mwaka jana kwa hivyo ana kibarua kigumu katika juhudi zake za kuibuka mshindi dhidi ya washindani kutoka Kenya Enock Onchari, Novestus Kirwa, Genicious Rono, Barnaba Kipkemboi, Lameck Too na Isaac Kipsang. Selly Kaptich, Pascalia Jepkogei, Viola Kibiwott na Emily Chebet watashiriki kitengo cha kinadada.

Itakuwa zamu ya bingwa wa Boston Marathon mwaka 2022 na 2023 Evans Chebet kuendea taji la tatu mfululizo. Atapata ushindani mkali kutoka kwa Wakenya wenzake Ronald Korir, Cybrian Kotut, John Korir, Albert Korir na Edward Cheserek na Mtanzania Gabriel Geay, Muethiopia Sisay Lemma, Mjapani Suguru, Mmoroko Zouhair Talbi na Sondre Moen kutoka Norway, miongoni mwa wengine.

Kitengo cha wanawake kimevutia Wakenya Edna Kiplagat,44, (bingwa wa 2017 na 2021), Judith Korir, Mary Ngugi-Cooper, Vibian Chepkirui, Helah Kiprop, Sharon Lokedi, Grace Kahura na bingwa mtetezi Hellen Obiri. Ushindani mkali katika kitengo hiki utatoka kwa Waethiopia na Waamerika.

Bingwa wa zamani wa marathon za Chicago na Boston Rita Jeptoo,43, ambaye anajivunia muda bora wa saa 2:19:57 atashiriki Zaragoza Marathon. Itakumbukwa alikosa mashindano kati ya 2014 na 2018 akitumikia marufuku baada ya kupatikana ametumia dawa za kusisimua misuli za aina ya EPO.