Kimataifa

Rubani alala na kupita uwanja wa kutua

November 27th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

NDEGE moja nchini Australia ilipita eneo ilipofaa kutua kwa kilomita 50, wakati rubani aliyekuwa akiiendesha kulala na kusahau kuielekeza kutua, maafisa wa usafiri wa hewani wamesema.

Hata hivyo, ni rubani huyo pekee aliyekuwa ndani ya ndege wakati wa tukio hilo, ambalo lilitokea mnamo Novemba 8.

Tukio hilo sasa limesababisha Halmashauri ya kusimamia Usafiri wa angani nchini humo (ATSB) kuanzisha uchunguzi kubaini kiini haswa cha kisa chenyewe ambacho kilihatarisha usalama.

Hata hivyo, maafisa hao bado hawajaeleza namna rubani huyo aliamka na kutuisha ndege yenyewe baadaye. Ilikuwa ikisafiri kutoka uwanja wa Devonport hadi kisiwa cha King, eneo la Tasmania na baadaye ilitua bila matatizo.

Wakati wa tukio hilo, ndege hiyo bado haikuwa imesafiri umbali wa kilomita 240.

“Rubani alilala na kufanya ndege hiyo kupita kisiwa cha King kwa kilomita 46,” ATSB ikasema kwenye habari yake.

ATSB ilisema kuwa itamhoji rubani huyo na kukagua namna ndege hiyo ilikuwa ikifanya kazi kabla ya kutoa ripoti mwaka ujao.

Mwaka uliopita, watu watano waliaga dunia wakati ndege waliyokuwa wakitumia kusafiri kuelekea kisiwa cha King ilianguka baada ya kupaa mjini Melbourne.