Habari Mseto

Rubia ashtaki serikali akitaka fidia ya Sh40bn

July 21st, 2019 2 min read

Na NYAMBEGA GISESA

ALIYEKUWA mfungwa wa kisiasa na mpiganiaji wa mfumo wa siasa za vyama vingi, Bw Charles Rubia, anaitaka serikali kumlipa fidia ya Sh40 bilioni kwa kufungwa gerezani na kudhulumiwa.

Kiasi hicho ndicho kikubwa zaidi nchini kuitishwa na mtu binafsi kama fidia.

Kwenye stakabadhi alizowasilisha katika Mahakama Kuu ya Nairobi wiki hii, Bw Rubia anaeleza kwa kina madhila aliyopitia katika miaka ya themanini na ya tisini kwenye harakati za kupigania demokrasia ya vyama vingi vya kisiasa.

Stakabadhi hizo ni za zaidi ya kurasa 200.

“Lengo letu ni kuona kuwa tumefanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa Bw Rubia amelipwa fidia kwa dhuluma alizopitia na ambazo hajawahi kulipwa hadi sasa,” akasema wakili wake, Seneta Irungu Kang’ata wa Murang’a kwenye mahojiano na Taifa Jumapili.

Bw Kang’ata alisema kuwa kiasi hicho si kikubwa, kwani hakuna fedha ambazo zinaweza kulipa dhuluma alizopata.

Bw Rubia anataka kulipwa Sh10 bilioni kwa hasara aliyopata, Sh20 bilioni kwa gharama ya matibabu na Sh10 bilioni ugumu aliokumbana nao akiwa gerezani.

Kando na hayo, anataka fidia ya Sh40 milioni kwa hasara ibuka na Sh150 milioni kwa hasara ya kibiashara aliyopata.

Anataka fedha hizo kulipwa kwa kuongeza riba kutoka Mei 1991 hadi siku atakayolipwa.

Bw Rubia alikuwa meya wa kwanza Mwafrika wa jiji la Nairobi. Vile vile, alihudumu kama mbunge na waziri kwa muda mrefu. Alifungwa gerezani mara mbili na serikali ya Rais Mstaafu Daniel Moi kwa kujihusisha katika harakati za kuitisha mfumo wa vyama vingi vya kisiasa.

Kwenye taarifa yake, Bw Rubia, aliye na umri wa miaka 95, anaeleza jinsi alivyopoteza thamani ya ubinadamu, hasa baada ya kufungwa gerezani.

Anaeleza kuwa mkewe alipata mshtuko na alifariki. Anasema kuwa licha ya kuwa na elimu nzuri, watoto wake walinyimwa ajira, huku yeye akiondolewa kama mkurugenzi katika kampuni kadhaa alizohudumu.

Zaidi ya hayo, kampuni mbalimbali ziliagizwa kutofanya biashara yeyote naye.

“Kila mmoja ambaye amepitia dhuluma za kisiasa anafahamu ugumu ambao huwepo. Imani yangu katika ubinadamu ilipotezwa kabisa na yale niliyopitia,” akasema.

Mnamo Februari 1987, Bw Rubia alikamatwa na kushtakiwa mwa madai ya kufadhili kundi la Mwakenya. Pia, alidaiwa kushirikiana na baadhi ya viongozi wa makanisa kupanga njama ya kununua bunduki ili kuipindua serikali.

Alisema kuwa serikali ilitumia asasi zake kumwibia kura kwenye uchaguzi wa 1988.

Mnamo Machi 3 1990, Rubia na aliyekuwa waziri Stanley Matiba waliita kikao na wanahabari katika jumba la Chester, Nairobi na kuitaka serikali kukubali vyama vingi vya kisiasa. Waliandaa mkutano wa amani katika uwanja wa Kamukunji Julai 7, 1990.

Lakini kabla ya mkutano alikamatwa akiwa na Matiba na kuzuiliwa kwa miezi tisa.