Habari Mseto

Rufaa dhidi ya Mishi Mboko yafutwa

May 15th, 2018 1 min read

Na PHILIP MUYANGA

ALIYEKUWA mbuge wa Likoni, Bw Masoud Mwahima ameondoa notisi ya rufaa aliyokuwa ameweka kwa madhumuni ya kupinga uamuzi wa mahakama kuu wa kuthibitisha kuchaguliwa kwa Bi Mishi Mboko kama mbuge wa eneo hilo.

Mahakama ya rufaa hapo jana ilikubali kuondolewa kwa notisi hiyo ambayo huwa inawekwa mahakamani iwapo mtu anataka kukata rufaa akikosoa uamuzi wa mahakama kuu. Bi Mboko na Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) haikupinga kuondolewa kwa notisi hiyo ya rufaa.

Majaji wa rufaa Alnashir Visram, Wanjiru Karanja na Martha Koome walikubali ombi hilo la kuondolewa bila gharama yoyote.

Mahakama kuu ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na Bw Mwahima ya kupinga kuchaguliwa kwa Bi Mboko.

Jaji Eric Ogola alisema kuwa Bw Mwahima hakuwa ametoa ushahidi wa kutosha kuthibitisha madai ya hongo na kuhitilafiana na Fomu 35B.

Katika uamuzi huo, jaji alisema kuwa ingawa kulikuwa na dosari katika uchaguzi huo, dosari hizo zilikuwa ndogo mno na hazingeweza kutatiza matokeo ya uchaguzi.

“Mahakama hii imeshawishika ya kuwa uchaguzi wa Bi Mboko haukuwa wa kiholela,” alisema Jaji Ogola.

Wakati kesi hiyo ilipokuwa inasikilizwa, Bi Mboko alisema kuwa hakuhusika na ufunguaji wowote wa madebe ya kupigia kura wakati wa uchaguzi wa Agosti 2017.

Mbuge huyo aliiambia mahakama ya kuwa hakuwa afisa wa IEBC wala hakuratibiwa kisheria kutekeleza kazi za tume hiyo.

Kwa upande wake, Bw Mwahima aliimbia mahakama ya kuwa alikuwa ameona madebe ya kura bila vifungo rasmi katika kituo cha kuhesabu kura cha Likoni.

Bw Mwahima alisema kuwa alimwambia afisa wa kura katika eneo hilo kutoendelea na kuhesabu kura hadi dosari hizo ziangaziwe.