Rufina (Mama Silas) aelezea safari yake ya uigizaji

Rufina (Mama Silas) aelezea safari yake ya uigizaji

Na JOHN KIMWERE

Ni mwanabiashara na miongoni mwa waigizaji waliovumisha kipindi cha Maria kilichozoa umaarufu sio haba ndani ya mwaka mmoja uliyopita.

Kipindi hicho kilichokuwa kinazalishwa na kampuni ya Jiffy Pictures kilikuwa kilipeperushwa kupitia Citizen TV. Anasema alianza kushiriki filamu mwaka 2019 bila kutarajia lakini ni talanta anayopania kuikuza.

Sussy Onzoleh Malaki ambaye kwa jina la usanii anafahamika kama Rufina ama Mama Silas alikuwa kati ya washiriki walioibuka kivituo kikuu kwenye kipindi hicho kilichopigwa breki wiki kadhaa zilizopita.

”Sina budi kusema kuwa ulikuwa mpango wa Mungu maana sikuwahi fikiria kwamba ningeshiriki maigizo lakini niliposhiriki majaribio niliibuka kati ya wasanii walioteuliwa kushiriki kipindi cha Maria,” alisema dada huyu na kuongeza kuwa tangia utotoni mwake alidhamiria kuwa mwana sheria (wakili).

Mwanamke huyu anasema kuwa kwa muda mrefu amekuwa akifuatilia filamu za Kinigeria (Nollywood). Anaongezea kuwa ingawa ameanza kushiriki maigizo akiwa na umri mkubwa wa miaka 48, anahisi anatosha mboga kushiriki filamu nyingi tu maana ameichukulia kama ajira.

Rufina anayejivunia kushiriki kipindi cha Maria pekee anasema anatamani apate kazi zingine za uigizaji ili apalilie talanta yake akilenga kutinga upeo wa kimataifa.

Anadokeza kuwa ingawa ndio ameanza kupiga ngoma kwenye gemu analenga kufikia hadhi ya mwigizaji mahiri mzawa wa Nigeria, Patience Ozokwor maarufu Mama G aliyeshiriki filamu kama ‘Blood Sister’ na ‘Chief Daddy,’ kati ya zingine.

”Kiukweli nimegundua kuwa wakati wa Mungu hakuna anayeweza kuuzuia maana sikutambua kama nina kipaji cha uigizaji lakini mwishowe nimejipata katika jukwaa hilo,” akasema.

Hapa nchini anasema angependa sana kufanya kazi na wasanii kama Madam Vicky aliyekuwa akishirikiana naye kwenye kipindi cha Maria. Pia angependa kufanya kazi na Celestine Gachuhi maarufu Selina ambaye hushiriki kipindi kiitwacho Selina ambacho hupeperushwa kupitia Maisha Magic.

Kwa waigizaji wa kigeni anasema kuwa angependa kutua jukwaa moja na wasanii kama Genevieve Nnaji bila kuweka katika kaburi la sahau Patience Ozokwor wazawa wa Nigeria.

Katika mpango mzima anamwomba Mungu amsaidie angalau ndani ya miaka mitano ijayo awe ameiva vizuri katika masuala ya maigizo. Kwa wasanii wanaokuja anawashauri watie bidii na watambue wanachotaka katika tasnia ya uigizaji.

PANDASHUKA

Mwigizaji huyu anasema hupitia kipindi kigumu hasa kuelewa sehemu yake kulingana na script katika filamu pia kushirikishwa na msanii anayeshindwa kuelewa mistari yake.

Licha ya hayo anasema tayari anaendelea kuimarika kila uchao wala hana matatizo kama ilivyokuwa mwanzoni. Anadokeza kuwa anajivunia kugundua ana kipaji cha uigizaji maana ndani ya mwaka mmoja mapato aliyopata yamemsaidia pakubwa kwenye shughuli za maisha.

You can share this post!

Otieno aelekea Kampala kutafuta tiketi ya Olimpiki ya mbio...

VALLARY ACHIENG: Ipo siku mtanitazama kwa runinga