Habari Mseto

Ruiru Girls yapata wafadhili ujenzi wa madarasa, mabweni

March 11th, 2020 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

KUNA haja ya kujenga mabweni ya wasichana hasa katika mji wa Ruiru ili wanafunzi wa kike wasipate shida ya kutafuta shule kwingineko.

Mbunge wa Ruiru Bw Simon King’ara alisema mji wa Ruiru una idadi kubwa ya wakazi na kwa hivyo ni vyema kujenga mabweni kadha ya wasichana ili wasije wakahangaika kutafuta shule katika maeneo mengine.

“Tayari nimepata malalamiko mengi kutoka kwa wazazi wakidai ya kwamba wana wao hasa wa kike wanalazimika kuhudhuria shule za kutwa jambo ambalo haliwafaidi sana kwa njia moja au nyingine,” alisema Bw King’ara.

Mnamo Jumanne, mbunge huyo alizuru shule ya upili ya Ruiru Girls Secondary ambayo ni ya kutwa na kutoa ahadi ya kujenga madarasa mawili kwa lengo la kutosheleza idadi ya wanafunzi wanaohudhuria shule hiyo.

Alisema tayari amefanya mazungumzo na wahisani kama ubalozi wa Japan na kampuni ya umeme ya Kenya Power ambao wameahidi kufadhili shule hiyo kwa fedha za ujenzi wa madarasa na mabweni kadhaa.

“Mimi mbunge wa eneo hili ninataka kuona ya kwamba kutoka muhula ujao shule hii inapata mabweni ya kutosha ili kuhifadhi wanafunzi wote wanaosoma na kurejea nyumbani kila mara. Hii itawapa nafasi ya kusoma bila kutatizwa kwa vyovyote vile,” alisema Bw King’ara.

Alisema sehemu kubwa ya kipande cha ardhi mji wa Ruiru imenyakuliwa na kwa hivyo tayari anafanya mipango na idara ya ardhi mjini Ruiru kuona ya kwamba vipande kama hivyo vinarejeshwa kwa umma mara moja.

“Ifikapo mwishoni mwa mwaka 2020 nitahakikisha vipande vya ardhi vimerejeshwa kwa umma kwa ajili ya matumizi muhimu. Mji wa Ruiru unazidi kupanuka na kwa hivyo ni vyema kuona ya kwamba ardhi ya umma inapatikana haraka,” alisema Bw King’ara.

Bi Sophia Waithera ambaye ni mwalimu mkuu wa shule ya upili ya Ruiru Girls Secondary alisema shule hiyo ina wanafunzi wengi na ni vyema akiongeza madarasa zaidi.

“Shule hii inapitia changamoto tele na kwa hivyo tunashukuru kupata usaidizi wa mbunge wetu wa hapa na pia tunawashawishi wahisani popote walipo wajitokeze kutusaidia,” alisema Bi Waithera.

Alisema tayari mipango inafanyika kuona ya kwamba ifikapo muhula ujao watakuwa wamepata mabweni ya wanafunzi hao ili waweze kusoma bila matatizo yoyote.

“Tunatamani pia kupata basi la shule litakalotusaidia kusafiri katika sehemu tofauti badala ya kukomboa matatu kila mara ambapo huwa ni ghali mno. Hata wazazi wanatamani kuona jambo hilo likitimia,” alisema Bi Waithera.

Alisema baada ya mabweni kujengwa shuleni mwalimu mkuu na naibu wake watapata nafasi nzuri ya kujumuika pamoja na wanafunzi katika eneo moja.

Alisema shule hiyo inajivunia kupata walimu wawili waliopokea tuzo ya kuinua wanafunzi wao katika masomo tofauti.

“Sisi kile tunaomba kwa sasa ni kupata usaidizi kutoka kwa wahisani ili kuona ya kwamba shule hii imepiga hatua zaidi,” alisema mwalimu huyo mkuu.