Habari Mseto

Rundo la taka latajwa sababu ya bodaboda kugongwa na kunusurika kifo

December 12th, 2020 1 min read

Na PETER CHANGTOEK

MWENDESHAJI mmoja wa pikipiki aliponea kwa tundu la sindano, baada ya kugongwa na gari lililokuwa likirudi nyuma, katika barabara ya Meru Road, Pumwani, Nairobi.

Kwa mujibu wa wale walioshuhudia kisa hicho ni kuwa, mwathiriwa huyo alikuwa akiiendesha pikipiki yake katika sehemu moja ya barabara hiyo, iliyokuwa imejazwa taka.

Rundo hilo la taka lilikuwa katikati ya barabara, na hivyo kuwalazimu waendeshaji magari na pikipiki kupitia sehemu moja nyembamba, ambayo ilikuwa imesalia barabarani.

“Gari hilo lilimgonga wakati ambapo lilikuwa likijaribu kurudi nyuma,” akasema mmoja wa wale walioshuhudia tukio hilo.

Jamaa huyo wa pikipiki alitumbukia mtaroni, na kugubikwa na maji taka, kabla hajaokolewa na watu waliokuwa karibu.

Wakazi wa eneo hilo walisema kutupwa hapo taka usiku husababisha magari na bodaboda kuwa na wakati mgumu kupitia sehemu hiyo.

Hata hivyo, uchafu huo ulizolewa mara baada ya tukio hilo.