Habari MsetoSiasa

Rungu la Moi sasa launganisha ‘vitoto vya kifalme’ nchini

February 13th, 2020 2 min read

Na BENSON MATHEKA

KUTEULIWA kwa Seneta wa Baringo, Gedion Moi kumrithi kisiasa baba yake Daniel Moi, na kauli ya ndugu yake Raymond kumtaka ashirikiane na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM Raila Odinga, kumefufua mjadala wa watatu hao waliozaliwa katika familia tajiri na zenye ushawishi kuendelea kuteka siasa za Kenya.

Wakati wa mazishi ya Mzee Moi eneo la Kabarak mnamo Jumatano, Bw Raymod Moi alitangaza kuwa familia ya baba yake, aliyekuwa rais wa pili wa Kenya, imemteua Gedion kuwa msemaji wake katika masuala ya kisiasa.

Alimtaka aimarishe chama cha Kanu na kukitumia kuunganisha Wakenya wote. “Sote tunaunga BBI nyuma ya Rais Kenyatta na Bw Odinga,” alisema mbunge huyo wa Rongai.

Gedion, kitinda mimba wa hayati Moi, alikubali wadhifa huo na atajiunga na Rais Uhuru ambaye ni msemaji wa familia ya Jomo Kenyatta aliyekuwa rais wa kwanza wa Kenya, na Raila mwana wa aliyekuwa makamu wa rais wa kwanza wa Kenya, Jaramogi Oginga Odinga.

Wadadisi wanasema hii inaashiria kujiri kwa muungano mkubwa wa kisiasa unaoshirikisha familia za Moi, Odinga na Kenyatta.

“Familia za Moi, Odinga na Kenyatta zina ushawishi mkubwa wa kisiasa nchini na chini ya BBI, zinaweza kuungana kuteka siasa za Kenya kwa miaka mingi,” asema wakili Thomas Maosa.

“Mbali na siasa, zina ushawishi wa kifedha na kimaeneo na wanasiasa wengine wenye majina makubwa walihusiana kwa njia moja na familia hizi,” aliongeza.

Bw Odinga ndiye kigogo wa kisiasa eneo la Nyanza, wadhifa aliorithi kutoka kwa baba yake, naye Uhuru ndiye msemaji wa eneo la Mlima Kenya ambalo baba yake alimiliki kwa miaka mingi hadi kifo chake. Kwa miaka mingi, Daniel Moi alikuwa kigogo wa siasa eneo la Rift Valley.

Naibu Rais William Ruto amekuwa akiwalaumu wakosoaji wake kwa kumpuuza kwa sababu hatoki familia zenye ushawishi. Akihutubia waombolezaji wakati wa mazishi ya Mzee Moi, Bw Odinga alipuulizia mbali madai kuwa familia za baba zao ni za kifalme akisema Moi, Odinga na Jomo Kenyatta walitoka familia maskini.

Wadadisi wanasema kwamba familia hizi zikiungana, itakuwa vigumu kubanduliwa uongozini.

“Vigogo wengine wa kisiasa nchini, akiwemo Bw Ruto walijengwa na familia hizi. Ruto alijengwa kisiasa na Moi lakini akakimbia mbio na kusahau Kenya ina wenyewe,” aeleza Bw Maosa.

Kulingana na wakili huyu, muungano wa familia hizi tatu unaweza kuzamisha azma za wanasiasa wengi, akiwemo Dkt Ruto. “Muungano wa familia hizi unaweza kuangamiza maisha ya kisiasa ya wasioelewa upepo wa siasa unavyovuma na wanaojiamini kama Dkt Ruto.”

Vigogo wa kisiasa kutoka maeneo mengine nchini kama vile Kalonzo Musyoka kiongozi wa chama cha Wiper, Musalia Mudavadi wa chama cha Amani National Congress, Moses Wetangula wa Ford Kenya na Ali Hassan Joho ambaye ni msemaji wa eneo la Pwani wameamua kuunga BBI.

“Kufaulu kwa viongozi hao kisiasa kulichangiwa na familia za Moi, Kenyatta na Odinga. Wanaelewa ni vigumu kuzipuuza na wanacheza kwa mbali kwa sasa,” anaeleza.

Mchanganuzi wa siasa, Bw Peter Gichara, anasema kuvunja ushawishi wa familia hizi ndio utakuwa mwisho wa ukoloni.

“Familia hizi hazina mapya kwa Wakenya kwa sababu zilifunzwa na wakoloni. Kuvunja ushawishi wao katika siasa za Kenya itakuwa ni kumaliza ukoloni kabisa. Kufanya hivi kutakuwa mwanzo wa kujenga demokrasia halisi,” aliongeza.