Makala

Runinga ina uwezo wa kuvunja ndoa?

July 25th, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

RUNINGA ni kifaa muhimu katika nyumba yoyote ile kwa kuwa itakupa burudani, elimu na uhamasisho.

Lakini kuna vipindi ambavyo huandaliwa na waendeshaji ratiba katika runinga hizo, ambavyo vimetajwa kuwa hatari kwa ndoa.

“Sio tu kwa ndoa bali ni kwa kila safu ya maisha. Kuna vipindi hatari kwa malezi ya watoto; vingine hatari kwa harakati za kidini… Wewe umeniuliza kuhusu ndoa. Ndio, wakati mume au mke ametekwa nyara na hivyo vipindi na kuvifuatilia hadi usiku wa manane na hivyo basi kumwacha mpenzi wake akisononeka kwa kitanda cha ndoa, runinga inakuwa inajenga au inabomoa?” anahoji mshauri wa masuala ya kifamilia, Bi Ann Muratha.

Anasema njia mwafaka ni kutema utumwa kwa vipindi hivyo na ikiwa ni lazima uvizingatie, basi muelewane na mpenzi au mchumba kuwa ama ni sawa ubakie hadi usiku wa manane ukivitazama au mvitazame wote wawili mkiwa na runinga ndani ya chumba chenu cha malazi ndio hali ikibidi, mko karibu na tunda lenu,” anasema.

Lakini sanasana wanaume huripotiwa kutekwa nyara na masuala mengine mbali na runing kama ulevi na biashara huku wake wakiripotiwa kuwa watumwa zaidi wa vipindi vya runinga.

Kwa mfano, aliyekuwa mbunge wa Mathioya Bw Clement Wambugu Muchiri ambaye kwa sasa hujishughulisha na masuala ya kujamii katika Kaunti ya Murang’a anateta kuwa mfumo mpya wa kidijitali katika maandalizi ya vipindi vya runinga unawapotosha wanawake wengi katika ndoa kwa kuwageuza kuwa wazembe.

Mwanamke afuatilia kipindi cha runinga. Picha/ Mwangi Muiruri

Anasema kuwa angekuwa na uwezo wa kipekee kama mtu binafsi, angepiga marufuku baadhi ya vipindi ambavyo vimewateka nyara fikira za wake wengi “ambao hukesha na kushinda kwa runinga wakifuatilia vipindi ambavyo havina manufaa yoyote kwa maisha yao.”

Anasema kuwa kuna baadhi ya vipindi ambavyo huwa vimepambwa kupotosha kuhusu utamu wa ndoa na ambapo utajiri, uwezo wa kingono na kukubali kwa wanaume kuosha nguo na vyombo hupigiwa debe kama ishara tosha za mwanamke kupendwa na mumewe.

“Hilo haliwezekani Afrika. Ukidai utumishi kama huo kutoka kwa mumeo basi utaishia kujipa talaka… Utasababisha mgogoro mkuu ndani ya boma lako. Hufai kuzingatia jumbe kama hizo katika sinema hizo za runinga,” anasema.

Anadai kuwa baadhi ya vipindi hivyo hasa vile vinavyohusisha waigizaji kutoka taifa la Nigeria almaarufu Afro Sinema ni hatari kwa walio katika ndoa.

Bw Wambugu anasema wakati umefika vipindi viwe vikidhibitiwa ili vile tu vinavyodumisha elimu ya maana kwa umma vitiliwe mkazo.

Bw Wambugu alifafanua kuwa vipindi hivyo vimewateka mabibi wengi na huwa wanavitazama hadi usiku wa manane huku mabwana zao wakisononeka kwa kuchapwa na makali ya baridi vitandani.

“Hali hiyo ni hatari sana kwani huvunja ndoa polepole na hata maadili mengi ambayo huwa katika sinema hizo hayana maana yoyote katika ndoa,” anasema.

Anasema wanawake huenda kulala wakati waume washachoka kuwangoja na hali hiyo huchangia hata uzinifu katika ndoa.

“Sasa, mke akikaa sebuleni akitazama vipindi vya Kizungu na pia vingine vya Afro Sinema ambavyo huangazia uchawi, maana yake kwa ndoa ni gani? Vijana wakienda kwa vyumba za Sinema kutazama filamu za ujambazi, vita na upelelezi, watajiinua na nini kimawazo na kimaisha?” akahoji.

Aliwapa changamoto wasanii wa hapa nchini waigize filamu ambazo zinavutia kwa maadili ya kijamii na ambazo zinaweza kuwakuza watazamaji kimawazo.

“Ni jambo la maana ikiwa sekta yetu ya usanii wa filamu itajiwakilisha kwa uzalendo wa kuichochea jamii kusonga mbele hasa kimapato, kimawazo na kimaadili. Pengo hilo ndilo limejazwa na filamu kutoka nje ambazo ukijaribu kutafuta maudhui yanayofaa mabibi na vijana wa Kenya hupati,” anakejeli.

Bw Wambugu anasema cha maana kwa sasa ni vijana wakimbilie michezo kama burudani lakini wasisahau maisha yanasonga mbele na kuna haja ya kujijenga kimapato.