Michezo

Runinga ya KTN kupeperusha gozi la Gor dhidi ya Zoo

February 14th, 2018 3 min read

Na CHRIS ADUNGO

Kwa Muhtasari:

  • Mechi hiyo itakayotandazwa uwanjani Kericho Green itakuwa ya kwanza ya Gor Mahia kuonyeshwa runingani
  • Gor watapania kutumia mchuano huo dhidi ya Zoo Kericho kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya KPL
  • Zoo Kericho ambao walidhalilishwa 4-2 na Ulinzi Stars ugani Afraha, Nakuru wanalenga kujinyanyua dhidi ya Gor Mahia

MCHUANO wa Ligi Kuu ya KPL unaotarajiwa kuwakutanisha kesho Zoo Kericho na Gor Mahia ambao ni mabingwa watetezi wa taji hilo, utapeperushwa moja kwa moja kupitia runinga ya KTN kwa ushirikiano na kampuni ya Mediapro kutoka Uhispania.

Mechi hiyo itakayotandazwa uwanjani Kericho Green kuanzia saa kumi alasiri Alhamisi itakuwa ya kwanza ya Gor Mahia kuonyeshwa runingani tangu kupulizwa kwa kipenga cha kwanza cha kuashiria mwanzo wa kampeni za Ligi Kuu msimu huu.

Awali, kipute hicho kilikuwa kimeratibiwa kusakatwa kuanzia saa tisa alasiri.

Gor Mahia ambao waliwakomoa Zoo Kericho 1-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa KPL msimu jana walilazimishiwa sare ya 1-1 na kikosi hicho katika mechi ya mwisho iliyowakutanisha uwanjani Kericho Green mwaka uliopita.

Chini ya kocha Dylan Kerr, Gor Mahia wanaingia katika mchuano wa Alhamisi wakijivunia hamasa ya kuwabamiza Leones Vegetarianos ya Equatorial Guinea kwa mabao 2-0 katika kivumbi cha Klabu Bingwa Afrika (CAF Champions League) kilichowakutanisha mjini Machakos mwishoni mwa wiki iliyopita.

Aidha, wapambe hao wa soka ya humu nchini watapania kutumia mchuano huo dhidi ya Zoo Kericho kurejea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya KPL baada ya kuanza vyema kampeni za msimu huu kwa kuwalaza Nakumatt 4-0 katika mechi yao ya kwanza iliyotandazwa mjini Machakos mnamo Februari 3, 2018.

      Pia waweza kupendezwa na habari hizi:

 

Nafasi ya 5

Alama tatu zilizovunwa na Gor Mahia katika mchuano huo kwa sasa zinawaweka katika nafasi ya tano kwenye jedwali linaloongozwa na mabingwa wa KPL 2008, Mathare United ambao waliwabamiza limbukeni Vihiga United 2-1 mnamo Februari 4 kabla ya kusajili matokeo sawa na hayo dhidi ya Nzoia Sugar mwishoni mwa wiki jana uwanjani Kenyatta, Machakos.

Bandari, Chemelil Sugar na Kariobangi Sharks wanakamilisha orodha ya vikosi vinavyounga mduara wa nne-bora baada ya kujizolea jumla ya alama nne kila mmoja kutokana na michuano miwili ya ufunguzi wa kampeni za msimu huu.

Kwa upande wao, Zoo Kericho ambao walidhalilishwa 4-2 na mabingwa mara nne wa KPL, Ulinzi Stars katika mchuano uliowakutanisha ugani Afraha, Nakuru mnamo Februari 3 wanalenga kujinyanyua dhidi ya Gor Mahia ambao walijishughulisha vilivyo katika muhula uliopita wa uhamisho wa wachezaji kwa maazimio ya kutia fora katika kampeni za soka ya humu nchini na mechi za kimataifa za CAF.

Hadi kufikia sasa, Zoo Kericho wananing’inia padogo kwenye mkia wa jedwali la KPL na kwa pamoja na Nzoia Sugar ambao wamepoteza michuano yote miwili ya ufunguzi, ndivyo vikosi vya pekee ambavyo havina alama yoyote kapuni mwao hadi kufikia sasa.

 

Kileleni

Ushindi kwa Gor Mahia utawarejesha kileleni mwa jedwali kwa alama sita sawa na Mathare ila watawapiga kumbo vijana hao wa kocha Francis Kimanzi kutokana na wingi wa mabao.

Zoo Kericho nao watachupa hadi nafasi ya 10 jedwalini iwapo watawachapa Gor Mahia kwa zaidi ya mabao mawili bila jibu.

Bandari ambao walinyanyua ubingwa wa Ngao ya GOtv mnamo 2015 wanashikilia nafasi ya pili baada ya kuambulia pointi moja kutokana na sare tasa dhidi ya Chemelil Sugar.

Bandari wamezoa alama nne, mbili nyuma ya Mathare United. Chemelil na Kariobangi Sharks, ambao wameruka juu nafasi moja na tatu mtawalia, pia wamejizolea alama nne kila mmoja ila wanatofautiana kwa ubora wa magoli.

Sharks walidondosha alama mbili muhimu katika sare ya 2-2 dhidi ya Vihiga United mwishoni mwa wiki jana. Gor Mahia hawakupiga mechi yao ya pili ligini kutokana na majukumu ya kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Afrika.

Migongo ya masogora hao wa Kerr inasomwa kwa karibu na Ulinzi Stars ambao walishuka nafasi tatu baada ya kuchapwa 1-0 na SoNy Sugar waliotawazwa mabingwa wa KPL kwa mara ya mwisho mnamo 2006.

Ulinzi wanasalia na alama tatu walizozivuna kutokana na ushindi wao wa 4-2 dhidi ya Zoo Kericho.