Habari Mseto

Runinga zajizima maeneo ya Mlima Kenya, Signet yaahidi kuamsha mitambo 

February 6th, 2024 1 min read

NA MWANGI MUIRURI

WENYEJI na wakazi wengi wa eneo la Kati wako gizani bila kupata vipindi vinavyopeperushwa kwa runinga kufuatia kuanguka kwa mitambo ya Signet, jukwaa linalotumika kupeperusha vipindi bila malipo.

Mnamo Jumanne walio na runinga wamebaki wakitumbulia macho skrini za runinga zikionyesha tu ilani ya “No Signal” yaani “Hakuna Mawimbi” kuashiria kulikuwa na hitilafu ya kimitambo.

Kwa sasa wako katika giza totoro la kupata vipindi vya elimu, burudani, na habari katika runinga zao.

Wengi ambao wamemweleza mwandishi wa Taifa Leo kuhusu mafadhaiko yao kufuatia hitilafu hiyo.

Walisema huduma hizo zilipotea mnamo Jumatatu.

“Hii imekuwa kawaida kwa kuwa kila mwezi lazima kuwe na siku kadha za hitilafu hii. Ni kana kwamba kuna msukumo fiche wa kuhamishia wamiliki wa runinga hadi kwa vipindi vya kulipia,” akasema Bw James Njoroge aliyepiga simu kutoka mji wa Murang’a.

Lakini Mhandisi wa Signet Fred Muia alisema kwamba hitilafu hiyo imekuwa ikitatiza lakini inatafutiwa jibu.

Alisema shida hiyo imekuwa ikijirejea tangu 2017.

“Ni suala la miundombinu katika mkondo wa upeperushaji. Ni hitilafu ambayo inahitaji ukarabati wa kina. Hii hitilafu huwa inatukumba lakini inashughulikiwa. Huwa ni shida ambayo ikikaa zaidi huwa ni ya wiki moja,” akasema Bw Muia.