Rupia arejea nchini baada ya kukatiza mkataba Saudi Arabia

Rupia arejea nchini baada ya kukatiza mkataba Saudi Arabia

NA JOHN ASHIHUNDU

Aliyekuwa mshambuliaji wa AFC Leopards, Elvis Rupia amerejea nyumbani baada ya kukatiza mkataba wake na klabu ya Al Bisha ya Saudi Arabia.

Rupia alijiunga na klabu hiyo miezi mitano iliyopita baada ya kutia fora akiisakatia AFC Leopards kwenye ligi kuu msimu uliopita.

Habari zaidi zimesema kwamba mshambuliaji huyo alikuwa miongoni mwa wachezaji wa kutimuliwa na Bisha baada ya klabu hiyo kulemewa ligini nchini Saudi Arabia.

Bisha imeshinda mechi tatu, kutoka sare mara tatu na kushindwa mara 14 kutokana na mechi 20 tangu staa huyo mwenye umria wa miaka 26 ajiunge na klabu hiyo.

Kabla ya kutwaaliwa na Bisha kwa mkataba wa miaka mmoja, Rupia alikuwa akiwindwa na watetezi wa ligi, Tusker.

Aliondoka baada ya kuifungia Leopards mabao 17 msimu uliopita, nyuma ya Erick Kapaito wa Kariobangi Sharks ambaye alitwaa tuzo ya mfungaji bora wa ligi msimu huo.

Alikuwa ameitwa kujiunga na Harambee Stars iliyokuwa ikijiandaa kwa mechi za mchujo wa kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, lakini akajiondoa baada ya kupata fursa hiyo ya kwenda Mashariki ya Kati.

Harambee Stars ilikuwa ikijiandaa kucheza na Uganda Cranes na Rwanda katika mechi hizo za kufuzu. Nafasi yake ilichukuliwa na Henry Meja ambaye yuko na klabu ya AIK ya Sweden kwa miaka mitano. Katika mechi hizo, Stars chini ya Ghost Mulee ilitoka sare 0-0 na 1-1.

  • Tags

You can share this post!

KWPL: Kangemi kuwinda ushindi wa kwanza ligini

Wakulima wa maembe hoi kampuni kukosa kununua zao

T L