Makala

Rusty Gee: Anatumia muziki kukabili matumizi ya mihadarati, ubakaji

March 2nd, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

INGAWA hajapata umaarufu katika jukwaa la muziki wa burudani anazidi kujibidiisha mithili ya mchwa kukuza kipaji chake katika utunzi wa nyimbo za kizazi kipya.

Tangu mwaka 2015 amekuwa akitumia muziki kupigana na matumizi ya mihadarati pia visa vya ubakaji.

Tunayezungumzia sio mwingine bali ni msanii chipukizi, Enock Wilson Teyie ambaye kimuziki anajulikana kama Rusty Gee.

”Nipo kwenye pilikapilika za kuandaa hafla ya kuzindua albamu yangu iitwayo ‘Mihadarati’ itakayofanyika mjini Luanda katika Kaunti ya Vihiga baadaye mwezi huu wa Machi,” asema na kuongeza kwamba Gavana wa Kaunti hiyo, Dkt Wilber Ottichilo ndiye atakayekuwa mgeni wa heshima kwenye uzinduzi huo maana wamekuwa wakijadiliana naye kuhusu hafla hiyo.

Kadhalika anadokeza kwamba amepania kushirikiana na Serikali ya Kaunti hiyo kuanzisha mradi wa kukuza talanta za wasanii chipukizi mashinani.

”Nilifikia uamuzi huo baada ya kugundua kwamba Kaunti ya Vihiga haijafanikiwa kupiga hatua kimuziki ilhali wapo wasanii wengi tu vijijini lakini hadi sasa hawajafaulu kupata mwelekeo wanavyoweza kuinuka,” aeleza.

Rusty Gee anasema analenga kudhihirishia wasanii chipukizi mashinani kwamba siyo lazima wahamie katika miji mikuu ili wafanikiwe katika muziki.

”Ninachofahamu ni kwamba wasanii chipukizi wanahitaji sapoti na mwelekeo hasa ni yapi ya kuzingatia ili kufanya vizuri katika muziki,” aeleza.

Msanii huyu amekuwa akishiriki hafla za muziki katika vyuo vikuu na taasisi tofauti nchini kuhamasisha jamii athari za kutumia mihadarati shughuli ambazo amekuwa akishirikiana na shirika la kukabiliana na matumizi ya  na Dawa za kulevya na vileo (Nacada).

Anasema amegundua uongozi wa Kaunti ya Vihiga unatambua masuala ya vijana hali inayompa nguvu kuishawishi ianzishe studio ya kurekodi tugho za wanamuziki chipukizi maeneo hayo.

Msanii Rusty Gee akiwa na Gavana wa Kaunti ya Vihiga Dkt Wilber Ottichilo. Picha/John Kimwere

”Nina imani hatua hiyo itafungua njia kwa vijana wengi wenye talanta lakini hawana uwezo kugharamia ada ya kurekodi nyimbo za utunzi wao watajitokeza na kuanza kukuza vipaji vyao,” asema.

Anasema analenga kujituma kwa udi na uvumba kuhakikisha anafanikiwa kutinga kiwango cha wanamuziki mahiri Afrika Mashariki kama Diamond wa Tanzania kati ya wengineo.

Albamu ya Mihadarati ina nyimbo 10 ikiwamo: ‘Mihadarati, ‘Usimnajisi’, ‘Bado tupo’, ‘Chanzo pesa’, ‘Kibera’, ‘Nyasaye’, ‘Kwenye Game’, ‘Rusty Gee’ ‘Mungu anaweza’, na ‘Hip hop’.

Rusty Gee aliyezaliwa katika kijijini cha Ebusiekwe, Kaunti ya Vihiga amefanikiwa kutembelea miji tofauti ikiwamo Kisumu, Nakuru, Mombasa, Kisii, Busia, Mumias na Eldoret.

Rusty Gee ni mtunzi wa nyimbo za kidunia lakini anasema anavutiwa na teke za injili kama ‘Hela’, ‘Utawala’ – kazi yake msanii na mtunzi wa hapa Kenya maruufu Juliani.

Pia anapenda kusikiza nyimbo zake Cannibal mwimbaji wa Mombasa kama ‘Kichwa Kibovu’, na ‘Street Hustler’.

Kwa muziki wa Bongo hupagawishwa na nyimbo zake Afande Sele ziitwazo ‘Mtazamo’, ‘Darubini kali’, pia fataki za ‘Hapo vipi’ ‘ Msinitenge’ zikiwa ni utunzi wake mwanamuziki anayefahamika kama Professor Jay.

Tangu ajiunga na muziki mwaka 2003 amefanya kazi na lebo nyingi tu katika maeneo tofauti nchini ikiwamo Alter Records, Ufuoni Records chini kinara wake Jeff Santana Films, Homesound, Double P music inayomiliwa na Magician na pia Grip Music chini ya prodyuza na mmiliki wake, Daddy Q inayopatikana jijini Nairobi.

Anashauri wasanii chipukizi wanaolenga kufanya vizuri kwamba mwanzo wanastahili kuonyesha nidhamu na kuelewa wanacholenga katika taaluma hii fana bila kuweka katika kaburi la sahau kwamba kukumbana na pandashuka ni jambo la kawaida.