Habari Mseto

RUTH KAMANDE: Muuaji mrembo aliyepata 'A' KCSE akiwa gerezani

July 19th, 2018 2 min read

Na WYCLIFFE MUIA

Kuna Wakenya wengi wamefungwa jela maisha ama kuhukumiwa kunyongwa kwa makosa mbalimbali. Lakini hukumu ya kifo Alhamisi dhidi ya Ruth Kamande ilikuwa inasubiriwa sana na wengi kwa sababu ya upekee wake.

Kwanza, hatua ya Bi Kamande kumuua mpenziwe mnamo Septemba 20, 2015 kwa kumdunga kisu mara 25 iliwashtua Wakenya wengi kwani kisa hicho kilionekana kama kilichovuka mipaka.

Jambo lingine lililofanya kesi hii kufuatiliwa kwa umakini na wengi ni kuwa mshtakiwa hakuwa tu mrembo kwa sura, lakini pia amedhihirisha kuwa mwerevu na gwiji masomoni.

Katika Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) mnamo 2015, Bi Kamande alishangaza wengi kwa kupata alama ya A- katika mtihani huo alioshiriki akiwa rumande.

Akiwa rumande, Bi Kamande aliamua kuendelea kukuza kipawa chake cha kuonyesha utanashati wake na Septemba 2016, alishiriki mishindano ya urembo magerezani na akaibuka mshindi kwa kuwabwaga wafungwa wengine 19 katika gereza la wanawake la Lang’ata.

Kutokana na umbo lake la nyungu na sura ya rangi ya noti ya ‘thao'(elfu moja), alitwikwa Taji la “Malkia wa Gereza la Wanawake la Lang’ata”.

Bi Kamande almaarufu ‘Biggy’ alisimulia mahakama jinsi walivyokabiliana na marehemu kuhusu ripoti ya afya ya mpenziwe ambayo alisema ‘ilimtisha’.

“Farid aliniambia ni heri aniue kisha ajiue badala ya kufichua hali yake ya kiafya. Baada ya kisu alichokuwa akinitishia nacho kuteleza na kuanguka kifuani mwangu, nilimdunga mara kadhaa ili kujiokoa,” Bi Kamande alielezea korti.

“Iliniuma sana kufahamu kuwa mtu niliyempenda na kumwamini sana alipanga kuniharibia maisha yangu.”

Alisema baada ya kumdunga kisu mara kadhaa, ambayo alisema hangekumbuka ni mara ngapi, alikimbia jikoni na kuchukua maji kujaribu kumuokoa mpenziwe kutokana na majeraha.

Korti iliambiwa kuwa baadhi ya vitu vilivyopatikana ndani ya chumba kisa hicho kilitokea ni barua za kimapenzi zilizotumwa na mpenzi wa marehemu kutoka Amerika, simu iliyovunjwa pamoja na kisu kilichokuwa na damu.

Bi Kamande alidokeza awali kuwa anaendelea kuandika kitabu kuhusu maisha yake.