Ruto aahidi kuokoa Wakenya kiuchumi

Ruto aahidi kuokoa Wakenya kiuchumi

LEONARD ONYANGO na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto ameahidi kuchukua hatua za kukwamua Kenya kutokana na matatizo ya kiuchumi yanayoikumba wakati huu iwapo atachaguliwa kuwa rais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Dkt Ruto ameahidi kufanikisha ahadi hiyo kupitia kuinua kilimo, kuboresha mazingira ya biashara ndogo na wastani na kuboresha hali ya kimaisha ya wananchi wa pato la chini.

Mgombea huyo wa muungano wa Kenya Kwanza pia ameahidi kumaliza uhaba wa walimu, kutoa matibabu nafuu na kusahihisha makosa ya serikali ya Rais Uhuru Kenyatta.

Katika sekta ya Kilimo, Kenya Kwanza imeahidi kutoa mkopo wa gharama nafuu kwa wakulima kupitia vyama vya ushirika.

Kulingana na manifesto hiyo iliyozinduliwa katika uwanja wa Kasarani, Alhamisi jioni, serikali ya muungano huo pia itaanzisha mpango wa bima kwa wakulima na wafugaji.

“Wakulima watakuwa wakipokea fidia endapo mimea au mifugo yao itaangamizwa na kiangazi, au majanga mengine ya kimaumbile,” manifesto hiyo inaeleza.

Endapo Dkt Ruto atashinda, serikali pia itapunguza uagizaji wa vyakula kutoka nje huku ikipiga jeki uuzaji nje wa mazao kama vile kahawa, pareto, maua, makadamia, chai miongoni mwa mengine.

Kwa ujumla, Kenya Kwanza imeahidi kuwekeza jumla ya Sh250 bilioni katika mipango ya kupiga jeki sekta ya kilimo kati ya 2023 na 2027.

Katika kitengo cha biashara ndogo ndogo, serikali ya Kenya Kwanza imeahidi kupitisha sheria itakayohakikisha kuwa wafanyabiashara hao wanapata leseni kwa njia rahisi pamoja na kutengewa na maeneo ya kuendeshea biashara kwa urahisi.

“Tutashirikiana na serikali za kaunti kutenga maeneo maalum ya kufanyia biashara mijini kwa lengo la kuimarisha mapato ya wafanyabiashara wadogo,” manifesto hiyo inaeleza.

Kenya Kwanza pia imeahidi kutenga Sh50 bilioni kila mwaka kutoka hazina ya kitaifa, ambazo zitatolewa kama mikopo ya gharama nafuu kwa wafanyabiashara wadogo.

Kuhusu sekta ya afya, serikali ya Kenya Kwanza imeahidi kuwa itafadhili mpango wa utoaji afya ya kimsingi katika vituo vyote vya afya bila malipo, pamoja na kuanzisha hazina ya kitaifa ya matibabu ya maradhi sugu kama vile kansa, kisukari na kiharusi.

Kuhusu nyumba, Kenya Kwanza imeahidi kujenga nyumba 250,000 za gharama nafuu kila mwaka. Mpango huu utatekelezwa chini Hazina ya Kitaifa ya Nyumba. Pia wameahidi kuanzisha mpango wa mkopo wa nyumba kwa gharama nafuu.

Vile vile, manifesto hiyo imeahidi kupiga jeki sekta ya juakali ili iweze kutengeneza bidhaa bora za ujenzi.

Ili kuvutia vijana, Naibu Rais ameahidi kutoa huduma za bure za intaneti kote nchini pamoja na kuhakikisha asilimia 80 ya huduma za serikali zitatolewa kwa njia ya dijitali.

Kuhusu elimu, Dkt Ruto ameahidi kuajili walimu wapya 116,000 ndani ya miaka miwili akiingia madarakani ili kupunguza uhaba uliopo nchini.

“Serikali ya Kenya Kwanza itathmini upya mfumo wa elimu ili kuhakikisha kuwa mamilioni wasiofanya vyema darasani hawabaguliwi,” inasema manifesto hiyo ya Kenya Kwanza.

Tofauti na mpinzani wake Raila Odinga wa Azimio la Umoja One Kenya, ambaye ameahidi kutoa elimu ya bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, Dkt Ruto ameahidi kupunguza gharama ya elimu: “Tutapunguza gharama ya elimu ya vyuo vikuu kwa lengo la kuhakikisha kuwa wanafunzi wanaokamilisha elimu ya upili wanajiunga na vyuo vikuu. Serikali ya Kenya Kwanza itajenga vyuo vya ufundi katika maeneobunge 52 yaliyosalia ndani ya miaka miwili baada ya kuchukua hatamu ya uongozi.”

Wanafunzi watakaokamilisha masomo yao katika vyuo vya walimu, matibabu (KMTC) na vyuo vikuu nao watapewa mafunzo ya nyanjani na serikali huku wakilpwa mshahara kwa mwaka mmoja.

Serikali ya Kenya Kwanza pia imeahidi kuongeza kiasi cha fedha za kulisha wanafunzi shuleni haswa katika maeneo kame na mitaa ya mabanda.

Walimu watakaofundisha katika maeneo yaliyo na changamoto za ukame na usalama nao watalipwa mshahara mnono zaidi kwa lengo la kuwapa motisha, Dkt Ruto anaahidi.

Kuhusu wazee, Dkt Ruto ameahidi kuongeza idadi ya wazee wa miaka 70 na zaidi wanaonufaika na Sh2,000 kwa kila mwezi.

Walemavu nao watatengewa asilimia tano ya vibanda vya kuuzia bidhaa kote nchini huku biashara zao ikipunguziwa ushuru na kutengewa asilimia tano ya kandarasi serikalini.

Naibu wa Rais pia ameahidi kuanzisha uchunguzi dhidi ya serikali ya Rais Kenyatta ndani ya siku 30 baada ya kuapishwa kuhusu utekwaji wa serikali na magenge ya kibiashara.

Uchunguzi huo, kulingana na Kenya Kwanza, unalenga kufichua mabwanyenye wachache ambao wamekuwa wakijinufaisha na kandarasi serikalini huku mamilioni ya Wakenya wakiumia.

  • Tags

You can share this post!

Montreal yanyamazisha Seattle Sounders ligi ya MLS

Romelu Lukaku arejea Inter Milan kwa mkopo baada ya kuagana...

T L