Habari MsetoSiasa

Ruto aahidi wakazi wa Mwiki shule mpya

June 3rd, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

ENEO la Maguo, Mwiki, Kaunti ya Kiambu linatarajia kushuhudia kufunguliwa kwa shule nyingine ya msingi ya umma hivi karibuni.

Naibu wa Rais William Ruto Jumapili alisema hatua hiyo inalenga kupunguza msongamano wa wanafunzi katika shule ya Mwiki.

Shule hiyo iliyoko katika wadi ya Mwiki, eneo bunge la Ruiru, Kiambu, inakadiriwa kuwa na zaidi ya wanafunzi 3,000.

Dkt Ruto alitangaza kuwa tayari serikali imetenga kima cha Sh10 milioni kufanikisha mradi huo. Alisema ujenzi unatarajiwa kuwa umekamilika kwa muda wa miezi mitatu ijayo.

Alisema ardhi itakayositiri shule hiyo mpya tayari imepatikana.

“Serikali ya Kenya imeweka wazi sharti kila mtoto asome. Tunataka kupunguza msongamano wa watoto katika shule ya Mwiki kwa kuligawanya wengine waende Maguo. Tayari ardhi tumepata kupitia jitihada za mbunge wa Ruiru na gavana wa kaunti hii,” alieleza Dkt Ruto. Simon King’ara ndiye mbunge wa Ruiru, naye gavana wa Kiambu ni Ferdinand Waititu.

Shule ya msingi ya Mwiki imekusanya watoto kutoka eneo la Githurai, Mwiki, Maguo, Progressive na hata Mumbi na Mwihoko. Darasa moja linakadiriwa kuwa na zaidi ya wanafunzi 230.

Dkt Ruto alifichua ujumbe huo alipofanya ziara katika shule hiyo, ambapo alitoa mchango wa Sh5 milioni ili kufadhili ujenzi wa madarasa matano zaidi.

Ujenzi wa maghorofa mawili unaendelea, na Naibu wa Rais aliagiza uwe umekamilika kwa muda wa wiki tatu zijazo. Mbunge wa Ruiru Simon King’ara ndiye amekuwa akisimamia ujenzi huo, na alisema atatoa Sh2 milioni kutoka kwa hazina ya CDF ili kurekebisha madarasa yaliyochakaa na kuunda upya vyoo.

Ruto pia aliahidi kufadhili kurembesha mazingira ya shule hiyo.

Kulingana na mwalimu tuliyezungumza naye na aliyebana jina lake kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza na waandishi wa habari, alisema shule ya Mwiki imesongamana kupita kiasi ikizingatiwa nafasi yake ni ndogo.

“Imesitiriwa na ardhi yenye ukubwa sawa na uga wa kandanda. Tumekuwa na wakati mgumu hasa vipindi vya michezo,” akasema. Aghalabu, uwanja wa kandanda unakadiriwa kuwa na kimo cha mita 100 urefu na mita 60 upana.

Wazazi walipongeza hatua ya serikali kuunda madarasa zaidi na kufungua shule nyingine. Aidha, wanafunzi walionekana kufurahishwa na ziara ya Dkt Ruto na baadhi yao kupata fursa ya kumsalimu.

Shule hiyo inayoongozwa na Bw Joseph Kamau, mwalimu mkuu, ndiyo yenye idadi kubwa ya wanafunzi nchini hasa baada ya mfumo wa elimu bila malipo kuzinduliwa.

Si mara ya kwanza shule hiyo kuangaziwa kwa msongamano unaotatiza shughuli za masomo na hata kuiweka katika hatari ya mkurupuko wa maradhi kwa sababu ya upungufu wa vyoo.

Dkt Ruto alikuwa ameandamana na gavana Ferdinand Waititu na baadhi ya wabunge wa Kiambu akiwemo Simon King’ara na kadha kutoka Bonde la Ufa, na madiwani kadhaa wa Kiambu.