Ruto aahidi yaliyoshinda UhuRuto

Ruto aahidi yaliyoshinda UhuRuto

Na LEONARD ONYANGO

NAIBU Rais William Ruto ameanza kutoa msururu wa ahadi ya yale atafanyia raia wa Kenya akichaguliwa rais licha ya kushindwa kutekeleza nyingi za ahadi hizo chini ya serikali ya Jubilee.

Dkt Ruto jana Jumatano alisema jukumu lake la kwanza mamlakani iwapo atachaguliwa kuwa rais mwaka 2022 ni kuhakikisha vijana milioni 4 wamepata ajira.

“Jukumu langu la kwanza afisini litakuwa kutenga fedha zitakazowezesha vijana milioni 4 kupata kazi. Vilevile, nitabuni hazina maalumu ya kusaidia wahudumu wa bodaboda na mama mboga kuinua hali yao ya maisha,” akasema Dkt Ruto.

Alisema pia atafufua Miradi Mikuu Minne ya Jubilee (Big 4 Ajenda) – kuhakikisha Kenya inajitosheleza kwa chakula, kustawisha viwanda, huduma nafuu na bora za matibabu kwa wote na nyumba nafuu – ambazo yeye na Rais Uhuru Kenyatta waliahidi kutekeleza baada ya kuapishwa kwa muhula wa pili Novemba 2017.

Kabla ya uchaguzi wa Agosti 8, 2017, Rais Kenyatta na Dkt Ruto waliahidi kubuni nafasi za kazi milioni 1.7 kila mwaka.

Wawili hao pia waliahidi kubuni Benki ya Biashara ambayo ingetoa mikopo kwa biashara ndogo ndogo, wakiwemo bodaboda na mama mboga.

Nyingi ya ahadi hizo zimesalia hewa kwa kuwa bado gharama ya matibabu ingali juu, idadi ya vijana wasio na kazi imeongezeka na zaidi ya Wakenya milioni 2 wanahangaishwa na makali ya njaa katika kaunti 23 nchini.

Japo Dkt Ruto alionekana kutengwa serikalini tangu 2018, alikuwa na usemi mkubwa kati ya 2013 na 2017 lakini hakutumia fursa hiyo kutekeleza miradi anayoahidi sasa.

“Naibu Rais alidhibiti nusu ya baraza la mawaziri na angewatumia vyema kuhakikisha mambo anaahidi sasa yanatekelezwa wakati wa serikali ya Jubilee,” anasema Bw Javas Bigambo, mdadisi wa masuala ya kisiasa.

Naibu wa Rais jana Jumatano alisema atatekeleza miradi hiyo minne pamoja na mpango wake wa ‘Bottom-Up’ anaodai utaangamiza umaskini nchini.

Dkt Ruto anaonekana kuendesha kampeni zake kwa ujanja kwani amekuwa akijipigia debe kwa kutumia miradi ya serikali na Jubilee kama vile ujenzi wa barabara lakini akijitenga na dosari za utawala huo.

Alipozuru maeneo ya Ukambani na Nyamira hivi majuzi, Dkt Ruto aliorodhesha miradi tele ya maendeleo iliyotekelezwa na Jubilee huku akisema ilikuwa ishara kwamba yeye ni mchapakazi.

“Wapinzani wangu hawana mradi wa kuwaonyesha Wakenya licha ya kuwa serikalini kwa miaka mingi,” alinukuliwa.

Alisema kinara wa ODM Raila Odinga, Bw Kalonzo Musyoka (Wiper) na Musalia Mudavadi (ANC) wamekuwa serikalini kwa muda mrefu lakini hawajafanya lolote.

Alipokuwa katika eneo la Ukambani, Dkt Ruto alijipigia debe kwa kutumia mradi wa Sh42 bilioni wa Bwawa la Thwake ulioko katika Kaunti ya Makueni.

Dkt Ruto amekuwa akisisitiza kuwa juhudi za serikali kutekeleza ajenda kuu za serikali zilihujumiwa na ushirika baina ya Rais Uhuru Kenyatta na Bw Odinga mnamo Machi 2018.

Wakati wa sherehe za Mashujaa, Oktoba 20, 2021 Rais Kenyatta aliorodhesha mingi ya miradi aliyotekeleza katika muhula wake wa pili – hatua iliyofasiriwa kwamba, alikuwa akimjibu Dkt Ruto ambaye amekuwa akisema serikali haijafanya lolote tangu mwafaka wa ushirikiano, maarufu kama handisheki miaka mitatu iliyopita.

Rais Kenyatta ameshikilia kuwa atakabidhi mamlaka kwa kiongozi ambaye ataendeleza miradi aliyoanzisha.

Mnamo Septemba, Rais Kenyatta alipokuwa akizindua hospitali mtaani Kibra, Nairobi, alionekana kupigia debe Bw Odinga huku akisema ndiye ana uwezo wa kuendeleza miradi aliyoanzisha.

You can share this post!

Wijnaldum afungua akaunti ya mabao kambini mwa PSG...

Wakenya washauriwa wawe waangalifu machafuko yakishuhudiwa...

T L