Ruto aahirisha kikao cha wawaniaji wa Bonde la Ufa

Ruto aahirisha kikao cha wawaniaji wa Bonde la Ufa

Na VITALIS KIMUTAI

NAIBU Rais William Ruto jana Ijumaa aliahirisha ghafla mkutano aliokuwa amepangiwa kufanya na wawaniaji kutoka kaunti kumi za eneo la Bonde la Ufa, wanaotafuta tiketi ya chama cha UDA katika uchaguzi mkuu ujao.

Mkutano huo ulikuwa umepangiwa kufanyika Jumanne ijayo katika makazi yake, mtaani Karen, jijini Nairobi.

Dkt Ruto amekuwa akitumia makazi hayo kukutana na jumbe tofauti zinazomtembelea kutoka sehemu mbalimbali nchini.

Tangazo hilo lilitolewa Alhamisi na Katibu Mkuu wa chama hicho, Bi Veronicah Maina.

“Chama kimetangaza kuahirishwa kwa mkutano ambao ulikuwa umepangiwa kufanyika Oktoba 26. Tutatangaza tarehe mpya za mkutano huo hivi karibuni,” akasema Bi Maina.

Wajumbe walioalikwa kwenye kikao hicho walitarajiwa kutoka katika kaunti za Bomet, Kericho, Nandi, Uasin Gishu, Elgeyo Marakwet, Baringo, Samburu, Turkana, Pokot Magharibi na Trans Nzoia.

Hatua hiyo inajiri huku wasiwasi ukiibuka miongoni mwa wafuasi wa chama hicho kuhusu ikiwa shughuli za uteuzi zitakuwa huru na zenye haki.

Wawaniaji wengi wanataka hakikisho kutoka kwa uongozi wake kwamba hakutakuwa na mapendeleo kwa wale watakaojitokeza kuwania nyadhifa kama ugavana, useneta, ubunge na udiwani.

Kwenye ziara ya siku sita aliyofanya majuzi Pwani, Dkt Ruto alifanya kikao na wawaniaji kutoka eneo hilo.

Kwenye kikao hicho, aliwahakikishia hakutakuwepo na mapendeleo yoyote wakati wa zoezi hilo.

You can share this post!

TSC yafuta walimu 43 kwa ukosefu wa maadili

UMBEA: Penzi lina ladha ya kipekee, utamu, uchachu, uchungu...

T L