Habari Mseto

Ruto abainisha ni kwa msingi upi anaweza kuunga mkono kura ya maamuzi ya Katiba

May 23rd, 2019 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

NAIBU Rais, William Ruto Alhamisi amesema kuwa hataunga mkono wito unaotolewa kutaka kubadilisha Katiba ikiwa nia kuu ni ya kuunda vyeo vya kugawana mamlaka ya serikali.

Aidha, amesema kuwa Kenya ya sasa ni lazima ikombolewe kutoka kwa siasa za wachache kusaka makuu ya kugawana keki ya kitaifa hadi ziwe kuhusu manufaa ya Wakenya wote kwa ujumla.

“Wengi husema kuwa siko tayari kuungana na Wakenya katika kutekeleza kura ya maamuzi ili tubadilishe Katiba eti tupanue nyadhifa za ugavi mamlaka. Huo si uongo; siwezi nikaunga mkono kura ya maamuzi ambayo itaandaliwa kwa msingi huo,” akasema Ruto.

Ruto amesema siasa za kumfurahisha mtu fulani ndipo kuwe na amani zimepitwa na wakati.

Amesema kuwa ikiwa kura hiyo ya maoni itazingatia usawa wa ugavi wa raslimali, uthabiti wa gharama ya mishahara na pia usawa wa kijinsia katika ugavi wa mamlaka, basi ataiunga mkono.

Amesema siasa za utapeli, udalali na kupinduana kimamlaka ndizo hupewa kipaumbele katika ushindani wa Kenya akisema kuwa “nitasimama kuhesabiwa miongoni mwa waliozikataa na ikiwezekana, kuzizima.”

Ruto amesema siasa huwa katika msingi wa kusaka serikali na pia upinzani, akisema kuwa mtazamo wa kuingia katika ushindani ukitarajia tu kushinda uchaguzi ndicho kiini cha shida nyingi za siasa za Kenya.

Alisema kuwa ukishindwa kura na hatimaye unakimbizana na kujipenyeza ndani ya serikali “ndio nataja kama utapeli wa kisiasa dhidi ya mpigakura.”

Alisema kuwa wakenya wa kawaida mara nyingi hapa nchini huwekwa kando na masilahi yao, wakirejelewa tu kama kinga dhidi ya kuanguka kwa wanasiasa wa ngome zao.

“Ukishatumia Wakenya kukuweka kwa mamlaka, unawasahau. Ukiyumbishwa katika wadhifa huo, unamkimbilia tena mpigakura akunusuru kupitia maandamano na masharti. Unapata kwamba viongozi wanaendelea kuvuna matunda ya uhuru huku Mkenya wa kawaida akiendelea kuhangaika kutoka kipindi cha uchaguzi huu hadi uchaguzi mwingine. Huo ndio utapeli ambao nataka tuungane kupinga katika siasa za nchi hii,” akasema.

Amesema kuwa liwe liwalo, atajiunga na Wakenya wa kawaida kusaka kura ya maamuzi ambayo ina maono ya kuongeza lishe na utajiri kwa walalahoi bali sio ya kuzidisha manufaa ya viongozi.

“Ukitarajia Ruto ajumuike nawe katika kura ya kuunda nafasi zaidi za kazi katika ugavi wa serikali, niko nje kwa uhakika. Ukileta kura ya kupunguza mzigo na gharama kwa Mkenya wa kawaida na kumpa afueni ya pato, heshima na majivuno ya kuwa katika taifa huru, niko ndani kwa uhakika,” akasema.