Ruto abuni mbinu za raia kujitajirisha

Ruto abuni mbinu za raia kujitajirisha

RAIS William Ruto amechukua hatua ya kubomoa bajeti ya serikali ya mtangulizi wake Uhuru Kenyatta, akisema imefanya nchi kugeuka mtumwa wa madeni.

Rais Ruto alisema serikali inalazimika kukopa ili kufadhili matumizi yake ila sharti mtindo huo ukomeshwe.

“Mwaka huu, tulipangiwa kukopa Sh900 bilioni kufadhili bajeti yetu ya matumizi. Tunakusanya Sh2.1 trilioni ambazo tunatumia kulipa madeni na mishahara. Lazima tukomeshe tabia hii,” alisema.

Mnamo Juni 2022, serikali iliyoondoka ya Jubilee chini ya Rais Uhuru Kenyatta, ilisoma bajeti ya Sh3.2 trilioni na ilipanga kukopa Sh900 bilioni ili kujaza pengo kwa kuwa serikali hukusanya Sh2.1 trilioni, jambo ambalo Rais Ruto alisema halifai.

“Serikali haifai kukopa kufadhili bajeti ya matumizi. Ni makosa. Lazima turekebishe,” Rais alisema kwenye kikao chake cha kwanza cha pamoja cha wabunge na maseneta.

Alisema ameagiza Wizara ya Fedha kushirikiana na wizara za serikali kupunguza bajeti kwa Sh300 bilioni mwaka huu wa kifedha.

“Katika miaka mitatu ijayo, ni lazima tubadilishe hali hii na kurudi katika hali ambayo serikali inachangia katika juhudi za taifa za kuweka akiba kwa kupunguza matumizi yake kuwa chini ya mapato. Nimeagiza Wizara ya Fedha kushirikiana na wizara nyinginezo kutafuta njia za kuweka akiba ya Sh300 bilioni katika bajeti ya mwaka huu,” alisema.

Rais Ruto aliomba wabunge kusaidia serikali yake kutimiza ajenda zake kwa kupitisha sheria za kuhakikisha Wakenya wanaendelea kuweka akiba ili kujenga utajiri wao binafsi na wa nchi yao.

Miongoni mwa sheria hizo ni kuongeza mchango wa wafanyakazi kwa Hazina ya Taifa ya Malipo ya Uzeeni (NSSF) akisema Sh200 wanazochanga kila mwezi kwa wakati huu, haziwezi kuwahakikishia maisha mema baada ya kustaafu.

“Mchango duni wa Sh200 kwa mwezi ni sawa na Sh72,000 kwa zaidi ya miaka 30. Sio ajabu kwamba Wakenya wengi hukimbilia kuwekeza katika ploti na kuzidisha bei za ardhi na pia ulaghai wa ardhi. Tunanuia kubadilisha muundomsingi wetu kwa ‘kinga ya jamii’ ili uweze kufaidi watu wengi,” alisema Rais.

Ili kuhimiza wasioweka akiba kufanya hivyo, Rais Ruto alipendekeza kampeni inayolenga walio katika sekta ya jua-kali kuweka mpango wa kuweka akiba.

“Katika kila shilingi mbili ambazo wataweka katika mpango huo, hadi Sh6,000 kwa mwaka, serikali itachangia Sh1. Hii ni sawa na Sh3,000 kwa Sh6,000 kwa mwaka ambazo serikali itawapa wanaoweka akiba chini ya mpango huu,” akaeleza.

Dkt Ruto alisema serikali yake itabadilisha utozaji wa ushuru ili uwe kwa msingi wa utajiri.

“Mzigo wa ushuru unafaa kuakisi uwezo wa kulipa. Hii inaafikiwa zaidi katika mfumo ambao ushuru unatozwa utajiri, matumizi, mapato na biashara. Mfumo wetu wa sasa wa ushuru hautimizi hili. Tunalemea biashara kwa ushuru na kutoza utajiri ushuru mdogo. Tutapendekeza hatua za kuanza kuchukua mwelekeo unaofaa,” alisema.

Rais Ruto alipendekeza Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Kenya (KRA) ibadilishwe jina kuitwa Huduma ya Ushuru ya Kenya ( KRS) kama sehemu ya mabadiliko ya serikali yake katika ukusanyaji wa mapato.

Kuhusu wito wa wabunge kurejeshewa Hazina ya Ustawi wa Maeneo-bunge (NG-CDF) iliyoharamishwa na Mahakama, Rais Ruto alisema kuna njia za kikatiba za kuihalalisha kwa kuwa inatekeleza jukumu muhimu la kuimarisha maisha ya Wakenya.Aidha, aliahidi maseneta hazina ya kuwasaidia kupiga darubini serikali za kaunti.

  • Tags

You can share this post!

Ebola: Madereva na wageni Moi International Airport jijini...

Azimio wamsuta Rais kwa kukwepa suala la vita dhidi ya...

T L