Siasa

JAMVI: Ruto achora taswira mpya?

August 30th, 2020 2 min read

Na MWANGI MUIRURI

HATUA ya Naibu Rais Dkt William Ruto ya kuzindua misururu ya kukosoa utawala wa Jubilee ‘kuipa darasa’ kuhusu utawala bora imemwangazia kama anayelenga kurithi wajibu wa kiongozi wa ODM Raila Odinga ambaye kwa muda mrefu amekuwa amejipa nembo ya mtetezi wa mwananchi wa kawaida.

Dkt Ruto ambaye katika siku za hivi karibuni ameonekana kutengwa na Rais Uhuru Kenyatta na washirika wake sasa ameonekana kujipamba upya katika safari yake ya kurithi urais 2022 kupitia kutetea wananchi wa kawaida ambao wamekuwa wakilia kutelekezwa na upinzani ulioungana na Jubilee chini ya mwavuli wa handisheki.

Naibu Mwenyekiti wa Jubilee David Murathe anahisi ni wakati mwafaka wa Ruto kufanya mazoezi ya kuwa upinzani akisema “kura ya 2022 kwa uhakika itamtuma rasmi kuwajibikia wadhifa huo.”

Katika mahojiano na Taifa Jumapili, Bw Murathe alisema ule muungano ambao Rais na washirika wake wanasuka kujiandaa mwaka 2022 una nguvu za kumtupa Dkt Ruto hadi upinzani kwa kuwa “hatakuwa na uwezo wowote wa kuibuka na ushindi.”

“Jubilee tunamchukulia Dkt Ruto kama mpinzani kwa kuwa alipoelekezwa na Rais akome siasa za mapema alikaidi, akaanza kuwakusanya washirika wa Rais hasa wa Mlima Kenya hadi kwa mrengo wake binafsi na kuzindua misururu ya kumkosea heshima kiongozi wa nchi na sasa anachokifanya kukemea serikali ambayo yeye ndiye wa pili kwa mamlaka ni dhihirisho tosha kuwa ashaamua kuanza kuwa upinzani mapema,” akasema Bw Murathe.

Washirika wa aliyekuwa mbunge wa Gatanga Peter Kenneth waliambia safu hii kuwa Dkt Ruto sasa ameamua kusaka ‘talaka ya kisiasa’ na Rais kwa udi na uvumba.

“Badala ya afanye hekima ajiondoe kwa hiari, anachochea Rais amtimue ndio ajipe ufuasi wa kuhurumiwa… Ni upinzani rasmi ndani ya serikali na ameonekana sasa kukumbatia mwito wa Rais kuwa yeye na mrengo wake wa ‘Tangatanga’ sasa wako huru kucheza siasa wengine wakichapa kazi ya kuwafaa wananchi,” akasema aliyekuwa mbunge wa Maragua, Elias Mbau.

Mbunge wa Gatanga Bw Nduati Ngugi ambaye wikendi alitangaza kuunga mkono uwaniaji wa urais wa Bw Odinga akiwa na Kenneth kama mgombea mwenza alisema kuwa kwa sasa Dkt Ruto ameonyesha waziwazi kuwa angependa kuachishwa majukumu yake ya unaibu wa rais ndipo adhibiti upinzani “ambao amekuwa akiucheza tangu 2014.”

Hata hivyo, wabunge Ndindi Nyoro wa Kiharu, Kimani Ngunjiri wa Bahati na Alice Wahome (Kandara) pamoja na Rigathi Gachagua (Mathira) walipuuzilia mbali misimamo hiyo.

Nyoro alisema kuwa Dkt Ruto anajihusisha na umma huku washirika wa Rais na Odinga wakizingatia tu masilahi yao ya kisiasa na kiuchumi hivyo basi kumtenga Dkt Ruto ambaye ni mtoto wa asili ya ‘Wanjiku’ mtaani.

Rigathi aliteta kuwa matapeli wa kisiasa wanataka kumwangazia Dkt Ruto kama asiye na haki ya usemi na fikira na hafai kuongea hata wakati mambo yanaenda vibaya kuhusu utawala.

Ngunjiri na Bi Wahome na wakasema kuwa wamechoka kuangazia kuhusu ukiukaji wa haki za kimsingi za raia na sheria mikononi mwa siasa za Handisheki na Dkt Ruto ambaye ameonekaka na dunia nzima kutengwa akiongea, anaitwa mpinzani badala ya mtetezi wa Wanjiku.

Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen sambamba na mbunge wa Kapseret Oscar Sudi walisema kwamba mrengo wa Dkt Ruto hautajibizana na washirika wa Handisheki au wa Rais na Jubilee bali utazingatia tu kubakia na urafiki na wananchi wa kawaida ukiwavutia ili wawe watetezi wa Dkt Ruto 2022.

“Ukiamua kujibizana na hawa watu wa ‘Kieleweke’, Handisheki na makuhani wa Murathe utachoka tu bure. Ikiwa kutetea Wanjiku asinyanyaswe na kukandamizwa na udikteta unaokithiri sasa ndio kuwa upinzani, basi na iwe hivyo,” akasema Murkomen.