Habari za Kitaifa

Ruto aelekea Italia kwa ziara ya kikazi

January 28th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto Jumapili, Januari 28, 2024 aliondoka nchini kwa ziara rasmi Italia, kuhudhuria kongamano maalum la taifa hilo na mataifa ya Afrika.

Kongamano hilo litafanyika kwa siku mbili jijini Rome, na linalenga kuboresha ushirikiano baina ya Italia na Afrika.

Pia, linalenga kuipa Italia nafasi kueleza mpango ilio nao kwenye ushirikiano baina yake na Afrika.

Kongamano hilo la siku mbili litaangazia masuala muhimu kama utoshelevu wa chakula, utamaduni, elimu, mafunzo ya kiufundi, usalama wa kawi, ushirikiano wa kiuchumi, ustawishaji wa miundomsingi na juhudi za kukabiliana na ugaidi na ulanguzi wa binadamu.

Jumla ya marais 20 kutoka Afrika watahudhurua kongamano hilo, lenye kaulimbiu: “Daraja ya Ukuaji wa Pamoja.”

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed, alisema kuwa Rais Ruto atahutubu kwa kuangazia suala muhimu la usalama wa kawi.

Kwa sasa, Rais Ruto anahudumu kama mwenyekiti wa Kamati ya Viongozi wa Afrika kuhusu Mabadiliko ya Hali ya Hewa (CAHOSCC).

“Jukumu la Rais Ruto katika kamati hiyo linaonyesha umuhimu wa kutilia maanani suala la mabadiliko ya hali ya hewa kwenye mazungumzo hayo,” akasema Bw Mohamed.

Zaidi ya hayo, Rais Ruto amepangiwa kufanya mazungumzo maalum na Rais Sergio Mattarella wa Italia kuhusu ushirikiano baina ya Kenya na taifa hilo.