Ruto aeleza jinsi alivyofanikiwa kumiliki ardhi kubwa Taveta

Ruto aeleza jinsi alivyofanikiwa kumiliki ardhi kubwa Taveta

VALENTINE OBARA NA LUCY MKANYIKA

NAIBU wa Rais William Ruto, hatimaye ameeleza wazi jinsi alivyofanikiwa kumiliki sehemu kubwa ya ardhi katika Kaunti ya Taita Taveta.

Suala la umiliki wa shamba hilo la takriban ekari 1,000 limekuwa likitajwa sana katika kampeni za kisiasa katika kaunti hiyo, ambapo baadhi ya wapinzani wake hudai aliipata kwa njia haramu.

Akizungumza Jumanne alipokutana na wakazi na viongozi wa Taita Taveta wanaoegemea muungano wa Kenya Kwanza, Dkt Ruto alithibitisha ripoti ambazo zimekuwa zikienea awali kwamba alipokea sehemu hiyo ya ardhi kutoka kwa aliyekuwa mbunge wa Taveta, Bw Basil Criticos.

Dkt Ruto, anayewania urais kupitia Chama cha UDA, aliibua suala hilo alipokuwa akitaka kuwashawishi wapigakura kwamba yeye ni mwenyeji wa Taita Taveta.

“Aliniambia nimsaidie kulipa deni la AFC (shirika la kufadhili kilimo nchini) akanigawia shamba lake hapo karibu. Kwani mtanipimia hewa na mimi ni mtu wa kijiji hiki?” akauliza.

Katika mikutano ya Jumanne, Dkt Ruto alipokea maoni ya wakazi kuhusu masuala ambayo wangependa yatatuliwe kwa haraka.

Masuala yaliyotajwa na wakazi wa Taita Taveta ni kama vile hitaji la uongezaji thamani katika mazao ya kilimo, ufadhili wa mbinu za kisasa za kilimo, uboreshaji wa uchimbaji madini kwa wawekezaji wadogo, na upanuzi wa masoko.

“Haya masuala tumekubaliana, tumeandika, tukaweka sahihi. Zaidi ya hayo tunataka tuwe na mwongozo maalumu wa watu wa Taita Taveta,” akasema.

Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Gavana wa Kilifi, Bw Amason Kingi, na mwenzake wa Kwale, Bw Salim Mvurya, ambao sasa wameanza rasmi mikutano ya pamoja kumpigia debe Dkt Ruto katika uchaguzi wa Agosti.

Wawili hao walikuwa wameteuliwa pamoja na Mwakilishi wa Kike wa Taita Taveta, Bi Lydia Haika, kusimamia mipango ya siasa za muungano wa Kenya Kwanza katika ukanda wa Pwani.

Bw Kingi alidai kuwa,wakazi wa Pwani bado hawatanufaika kutoka kwa ODM hata kama Gavana wa Mombasa, Bw Hassan Joho, ametangazwa kupewa wadhifa wa waziri wa Ardhi endapo Azimio itaunda serikali ijayo.

Kulingana naye, kuna Wapwani wengi ambao wamewahi kushikilia wadhifa huo katika miaka iliyopita ila changamoto za umiliki wa ardhi bado zinakumba wakazi wa ukanda huo.

“Tunachotaka ni mipangilio bora ya serikali ambayo itawezesha mabadiliko,” akasema.

Kwa upande mwingine, Bw Mvurya alirai wakazi kuunga mkono Kenya Kwanza akisema njia hiyo ndiyo itahakikisha mabadiliko yanayopangwa na Dkt Ruto yatapatikana endapo atashinda urais.

“Nilipohama ODM kuingia Jubilee, watu wengi walilalamika lakini nilikuwa nimeona hakuna sera pale ndani. Mambo ya uchumi hayataki kiongozi ambaye amechoka,” akasema.

Bw Mvurya alihama ODM akajiunga na Jubilee mwaka wa 2017, kabla kuamua kuegemea Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kinachoongozwa na naibu rais.

Naye Bw Kingi alishinda ugavana mara mbili kupitia kwa ODM kabla kuunda chama cha Pamoja African Alliance (PAA).

Awali alikuwa ameongoza PAA kujiunga na Azimio lakini akahamia Kenya Kwanza baadaye pamoja na Dkt Mutua.

Dkt Ruto anatarajiwa kuzuru kaunti mbalimbali za Pwani wakati ambapo mvutano umeibuka baina ya viongozi wa vyama tanzu vinavyomuunga mkono.

  • Tags

You can share this post!

TUSIJE TUKASAHAU: Ruto alikuwa mstari wa mbele wakati...

Himizo wanaougua fistula wasake tiba

T L