Ruto afaulu kunusuru UDA baada ya mzozo kutatuliwa

Ruto afaulu kunusuru UDA baada ya mzozo kutatuliwa

Na BENSON MATHEKA

MZOZO ambao ulitishia kumpokonya Naibu Rais William Ruto chama cha United Democratic Alliance (UDA) umesuluhishwa.

Hii ni baada ya aliyekuwa mwenyekiti Bw Mohamed Noor kuondoa kesi aliyowasilisha mbele ya Jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa.

Bw Noor alikuwa amepinga ilani ya viongozi wapya wa chama hicho iliyochapishwa na msajili wa vyama vya kisiasa ambaye alitambua washirika wa Dkt Ruto kuwa viongozi halali wa chama hicho.

Akiondoa kesi hiyo, alisema kuwa ameridhika na uamuzi wa msajili wa vyama kupitia ilani aliyochapisha Machi 19 akitambua washirika wa Dkt Ruto kuwa viongozi wa chama cha UDA.

“Mlalamishi ameridhika na uamuzi wa mshtakiwa kupitia ilani katika gazeti rasmi la serikali,” Bw Noor alisema kwenye makubaliano ya kumaliza mzozo huo.

Hatua hii inamaanisha kuwa aliyekuwa seneta wa Machakos, Bw Johnston Muthama angali mwenyekiti wa chama hicho, aliyekuwa seneta wa Kakamega, Dkt Boni Khalwale ataendelea kuwa Naibu mwenyekiti na Bi Veronica Maina atasalia kuwa katibu mkuu.

Watatu hao ni washirika wa kisiasa wa Dkt Ruto ambaye amekuwa akipigia debe chama hicho. Bw Muthama na Dkt Khalwale na washirika wengine wa Dkt Ruto wametangaza kuwa chama hicho ndicho Naibu Rais atatumia kugombea urais kwenye uchaguzi mkuu wa 2022.

Bw Noor alikuwa ameomba jopo kubatilisha uamuzi wa msajili wa vyama vya kisiasa wa kutangaza washirika wa Dkt Ruto kuwa maafisa wa chama hicho ambacho kimepata umaarufu kwa kutambulishwa na Dkt Ruto.

Kwenye kesi yake, aliomba jopo kumrejeshea umiliki wa chama cha UDA.Alilalama kwamba kuidhinishwa kwa washirika wa Dkt Ruto kuwa maafisa wa chama hicho, kulikuwa kinyume cha sheria.

Katika kesi aliyowasilisha mbele ya jopo la kutatua mizozo ya vyama vya kisiasa, Bw Noor alisema kwamba aliyekuwa katibu mkuu Mohammed Sahal ambaye aliidhinisha kubadilishwa kwa maafisa wa chama hicho, ni mtumishi wa umma na kwa hivyo hana mamlaka ya kufanya hivyo.

“Suala hili limesuluhishwa kati ya mlalamishi, mshtakiwa na waliohusishwa na kesi hiyo,” yalisema makubaliano ya kumaliza mzozo huo. Seneta wa Elgeyo Marakwet Kipchumba Murkomen, aliongoza washirika wa Dkt Ruto kufurahia hatua hiyo.

“Suala dogo kati ya Bw Abdi Noor Mohamed na UDA Kenya limetatuliwa kwa amani,” Bw Murkomen aliandika kwenye Twitter.

You can share this post!

JAMVI: Gavana Kingi aning’inia kisiasa Muungano wa...

Serikali italipa fidia ya Sh14 bilioni kwa walioshambuliwa...