Habari

Ruto ahepwa tena

June 1st, 2019 2 min read

Na RUTH MBULA na JOSIAH ODANGA

MAKAMISHNA wa Kaunti za Kisii na Nyamira Godfrey Kigochi na Amos Mariba, magavana na maafisa wakuu wa polisi, Ijumaa walisusia hafla za Naibu Rais William Ruto alipozuru kaunti hizo.

Magavana James Ongwae na John Nyagarama walikosa kuhudhuria hafla hizo za Dkt Ruto na kundi la wabunge wanaomuunga mkono, hali ambayo iliwaghadhabisha viongozi waliokuwa wameandamana naye na kuwakosoa.

Naibu Rais anafaa kupokewa na mshirikishi wa serikali wa eneo analozuru, kamishna wa kaunti ama kamanda wa polisi lakini katika maeneo hayo maafisa hao hawakuwepo Dkt Ruto alipozuru Kisii na Nyamira.

Hata hivyo maafisa hao hawakufika katika chuo cha mafunzo anuwai cha Nyagesa ambapo Ruto aliweka jiwe la msingi, alipofungua ofisi ya Hazina ya Eneobunge la Mugirango Magharibi na kuongoza harambee katika kanisa Katoliki la St Joseph Nyamira na SDA Borabu nyumbani kwa Dkt Matiang’i.

Viongozi wa eneo hilo, ambao walijumuisha wabunge Vincent Kimosi (Mugirango Magharibi), Ben Momanyi (Borabu), Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Joash Nyamoko (Mugirago Kaskazini), Mwakilishi wa Wanawake Nyamira Jerusha Momanyi, Sylvanus Osoro (Mugirango Kusini) na Innocent Obiri (Bobasi) walikosoa hatua ya maafisa hao kumkwepa Ruto, wakisema haifai hivyo.

Dkt Ruto, hata hivyo, hakuzungumza kuhusu tukio hilo, ambalo limekuja wiki chache tu baada ya visa sawa na hicho kushuhudiwa katika maeneo ya Nyeri na Turkana, hali ambayo iliibua tumbo oto.

Naibu Rais aliendelea na hafla zake Nyamira (kaunti ya nyumbani ya Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i) na Kisii, akitoa ahadi kuwa ataendelea kuzuru mashinani licha ya malalamiko kutoka kwa baadhi ya watu kuhusu ziara zake.

“Wananchi wengi wako mashinani na wanahitaji kuhudumiwa kama tu wale walio maofisini. Wakenya wanataka tuungane na tuelekeze mipango yetu yote katika maendeleo. Sikuja hapa leo kupiga siasa, hiyo ni kazi ya siku nyingine,” akasema Naibu Rais.

Aliendelea kusema kuwa Nyamira haitabadilishwa na siasa duni, ila viongozi ambao wanajali maendeleo.

Kuhusiana na kukosekana kwa Gavana Nyagarama, hata hivyo, katibu wa kaunti hiyo Eric Onchana alimtetea akisema watakutana na Dkt Ruto katika Kaunti ya Narok, wakati wa sherehe za Madaraka Dei leo.

Kukosekana kwa maafisa hao kulikuja siku kadhaa, baada ya Dkt Ruto kudaiwa kukorofishana na katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho katika uwanja wa ndege wa JKIA, walipokuwa wameenda kumpokea Rais Uhuru Kenyatta alipokuwa akirejea nchini kutoka ziara ya nje.

Lawama

Dkt Ruto alidaiwa kumzomea Dkt Kibicho akimlaumu kwa kutatiza shughuli zake (Dkt Ruto) kwa kuwakataza maafisa wa usalama katika maeneo tofauti kuhudhuria hafla zake.

Aidha, kumekuwa na ripoti kuwa kuna tofauti kati ya Naibu Rais na Waziri Matiang’i, tangu alipopandishwa cheo kuwa akiwasimamia mawaziri wenzake na Rais Uhuru Kenyatta, hatua ambayo baadhi ya watu waliifasiri kama pigo kwa Dkt Ruto.

Wiki chache zilizopita, afisi ya Rais iliwateua maafisa wawili na kuitaka ile ya Naibu Rais kuwa ikiwafahamisha kuhusu ziara za Dkt Ruto, ili kurahisisha shughuli za kufadhili usalama na kuwafahamisha makamishna wa kaunti kujipanga.

Miezi miwili iliyopita, wabunge wanaomuunga Dkt Ruto walilalamika kuwa walipokonywa walinzi na kumlaumu Bw Kibicho na Bw Matiang’i kufuatia hatua hiyo.