Habari Mseto

Ruto ahimiza mazungumzo kuhusu utata wa fedha

July 20th, 2019 1 min read

Na LILIAN MUTAVI na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amewahakikishia Wakenya kwamba juhudi zinafanywa kusuluhisha mvutano kuhusu ugavi wa fedha kwa serikali za kaunti nje ya mahakama.

Alielezea matumaini kuwa mabunge ya Kitaifa na Seneti hivi karibuni yataafikiana kuhusu kiwango cha pesa kinachopaswa kutengewa serikali za kaunti kuhakikisha shughuli za utoaji huduma hazikwami.

Akiongea Jumamosi katika kanisa la African Inland (AIC) la Katisaa, Mumbuni, Kaunti ya Machakos, Dkt Ruto alisema ni kupitia mazungumzo ambapo suluhisho kwa tatizo lolote linaweza kupatikana.

“Tunafanya kila tuwezalo kumaliza tofauti kati ya Seneti na Bunge la Kitaifa kuhusu ugavi wa pesa katika kaunti kwani suala kama hili linaweza tu kushughulikiwa kupitia kwa mazungumzo,” Dkt Ruto akasema.

Mwelekeo

Alisema si wajibu wa mahakama kuamua kiwango cha fedha zinazofaa kutengewa serikali za kaunti ila tu inaweza kutoa mwelekeo kuhusu namna suala hilo litashughulikiwa.

“Japo mvutano huu umewasilishwa mahakamani bado nina imani kuwa unaweza kutatuliwa kupitia kwa njia ya mazungumzo,” Dkt Ruto akaongeza.

Mnamo Alhamisi Baraza la Magavana (CoG) liliwasilisha suala hilo katika Mahakama ya Juu likitafuta ushauri na mwelekeo kuhusu suala hilo.

Magavana wanapinga hatua ya Bunge la Kitaifa na Hazina ya Kitaifa kuzitengea serikali za kaunti Sh310 bilioni pekee, kama ilivyo katika bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha Henry Rotich mnamo Juni 13.

Lakini CoG inayoongozwa na Gavana Wycliffe Oparanya inapendekeza mgao wa Sh335 bilioni namna ilivyopendekezwa na Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) na kuungwa mkono na Bunge la Seneti.