Ruto aingia hema la Mudavadi

Ruto aingia hema la Mudavadi

Na BENSON MATHEKA

NAIBU wa Rais William Ruto atatumia muungano ‘ulioundwa’ mwaka 2021 na kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Katika mkutano wa kisiasa uliofanyika jana jijini Nakuru, Dkt Ruto alisema chama chake cha United Democratic Alliance (UDA), ANC na Ford Kenya cha Bw Moses Wetang’ula vitakuwa chini ya muungano mpya wa Kenya Kwanza.

Alisema muungano huo utatoa kipaumbele kwa uchumi iwapo kundi lake litashinda urais na kuunda serikali Rais Uhuru Kenyatta atakapostaafu baada ya Uchaguzi Mkuu ujao.

“Kenya Kwanza ni muungano wa kulinda Katiba ya Kenya, si wa kutafuta maslahi yetu ya kibinafsi. Ninawaambia tumeungana na hawa wangwana (Mudavadi na Wetang’ula) kwa kuwa tuna mpango mzuri wa Kenya. Kundi hili mnaloona hapa limeungana chini ya mwavuli wa Kenya Kwanza ili kubadilisha uchumi na maisha ya Wakenya,” alisema Dkt Ruto.

“Urafiki wetu na viongozi wa kisiasa kutoka ANC, Ford Kenya na makundi mengine umejengwa katika imani thabiti kwamba ni lazima tuunganishe na kurejesha nchi yetu katika njia ya ustawi,” Dkt Ruto alisema Jumatano.

Naibu huyo wa rais alisema kuwa muungano wa Kenya Kwanza utapata ushindi kwa kishindo katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Hatua ya Dkt Ruto kuungana na Bw Mudavadi na Wetang’ula imechukuliwa kuwa sehemu ya mikakati mipya ya kumkabili kinara wa ODM Raila Odinga anayeungwa mkono na Rais Kenyatta kupitia vuguvugu la Azimio la Umoja.

“Mnavyoona tukiwa hapa, si uchaguzi wa 2022 umeisha asubuhi na mapema,” Dkt Ruto aliambia wafuasi wake.

Jina la ‘Kenya Kwanza’ lilihifadhiwa katika Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa mnamo Oktoba 2021 na wandani wa Bw Mudavadi.

Hatua hiyo ilisababisha waliokuwa vigogo wenzake wa muungano wa One Kenya Alliance (OKA) kumshuku Bw Mudavadi.

Jina la muungano wa OKA lilihifadhiwa na kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka.

Bw Mudavadi wikendi iliyopita alitangaza kugura muungano wa OKA – ambao sasa umesalia na Bw Musyoka na Seneta Gideon Moi (Kanu) – na kuungana na Naibu wa Rais Ruto.

Naibu wa Rais mnamo Jumatatu alisema kuwa wanaendelea kuandaa mkataba wa maelewano ambao baadaye watawasilisha kwa Msajili wa Vyama vya Kisiasa, Bi Ann Nderitu.

Mkataba huo utatoa mwongozo kuhusu jinsi vyama vya ANC, UDA na Ford Kenya vitakavyogawana nyadhifa serikalini endapo muungano wa Kenya Kwanza utashinda Uchaguzi Mkuu wa Agosti 9.

Jana Jumatano, Bi Nderitu aliambia Taifa Leo kuwa hajapokea maombi ya kusajili Kenya Kwanza kama muungano rasmi wa kisiasa.

“Kufikia sasa hakuna muungano ambao umesajiliwa rasmi. Walichofanya ni kutuma maombi ya kuhifadhi majina ya miungano yao,” akasema Bi Nderitu.

Dkt Ruto ameshikilia kuwa hataungana na vyama vidogo ambavyo anadai vinafadhiliwa na Rais Kenyatta na Bw Odinga.

Inaonekana Dkt Ruto ameanza kupanga upya kampeni zake uchaguzi mkuu ujao unapokaribia akitumia mbinu sawa ambazo yeye na Rais Kenyatta walitumia kujiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2013.

Sawa na walivyofanya 2013 kutangaza ndoa ya vyama vyao vya The National Alliance (TNA) na United Republican Party (URP) katika mkutano mkubwa mjini Nakuru wakijiandaa kumrithi Mwai Kibaki 2013, ndivyo alivyofanya jana alipoandaa mkutano wa kwanza wa kisiasa na washirika wake wapya, Mabw Mudavadi na Wetang’ula.

Ni katika mkutano mjini Nakuru 2013 ambapo Rais Kenyatta na Dkt Ruto walitangaza muungano wao wa Jubilee ulioleta pamoja chama vyao vya TNA na URP kukabiliana na muungano wa Coalition for Restoration of Democracy (CORD) uliojumuisha Bw Raila, Bw Musyoka na Bw Wetang’ula.

Uhusiano baina ya Dkt Ruto na Rais Kenyatta ulidorora katika muhula wao wa pili uongozini na akatengwa serikalini na katika chama tawala cha Jubilee alichotarajia kutumia kumrithi mkubwa wake ikulu na akaunda chama cha UDA.

Wadadisi wanasema kwamba japo alianza kampeni miaka minne iliyopita na kuvutia washirika kadhaa kutoka sehemu tofauti za nchi, Dkt Ruto atalazimika kusuka mikakati mipya ili kuwatosheleza washirika wake wote hasa baada ya mchujo.

Kwa miaka minne, Dkt Ruto alikuwa akifanya mikutano ya kampeni peke yake na jana ulikuwa mkutano wake wa kwanza kujumuisha washirika wake wapya.

Alikuwa amekataa kuungana na vyama kadhaa vya eneo la Mlima Kenya ikiwemo Chama cha Kazi cha mbunge wa Gatundu Kusini Moses Kurian a The Service Party of Kenya cha aliyekuwa Waziri wa Kilimo Mwangi Kiunjuri.

“Awali alikuwa amekataa kuingia katika miungano na vyama vya kisiasa lakini baada ya kukumbatia ANC na Ford Kenya, atalazimika kusuka upya mikakati yake ili kutosheleza idadi ya wawaniaji inayozidi kuongezeka ikiwa ni pamoja na washirika wake wapya,” asema mchanganuzi wa masuala ya siasa Derrick Khaosa.

Anasema katika kusuka upya mikakati yake, Dkt Ruto anafaa kuwa makini ili kulinda na kudumisha umaarufu ambao amejijengea katika miaka minne na kuepuka kurudia makosa yaliyozua mgogoro katika Jubilee.

You can share this post!

Hofu ardhi ya ekari 9,000 imenyakuliwa

Kabichi adimu na yenye soko mithili ya mahamri moto

T L