Ruto ainua mikono, asema yuko tayari kuridhiana na Uhuru bila masharti

Ruto ainua mikono, asema yuko tayari kuridhiana na Uhuru bila masharti

Na CHARLES WASONGA

NAIBU Rais William Ruto amesema kuwa yuko tayari kufanya mazungumzo na Rais Uhuru Kenyatta kwa lengo la kuridhiniana kisiasa, bila kuweka masharti yoyote.

Akiongea Alhamisi siku moja baada ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini kusema wako tayari kumpatanisha na Rais Kenyatta, Dkt Ruto alisema anamheshimu Rais ambaye alimtaja kama “bosi wangu”.

“Nimewasikia hawa maaskofu wakisema wanataka kunipatanisha na Rais. Ningependa kusema kuwa niko tayari kwa upatanishi huo bila masharti yoyote,” akasema.

Dkt Ruto alisema hayo Alhamisi alipohutubia ujumbe kutoka eneo bunge la Kandara uliomtembea katika makao yake rasmi, mtaani Karen, Nairobi. Ujumbe huo wa wafuasi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) uliongozwa na mbunge wa eneo hilo, Alice Wahome na Seneta wa Murang’a Irungu Kang’ata.

Naibu Rais alisema kuwa kuna watu wachache ambao alidai walichochea uhasama kati yake na Rais Kenyatta kwa malengo mabaya.

Mnamo Jumatano, Muungano wa Maaskofu wa Kanisa Katoliki Nchini (KCCB), walisema wamejitolea kupatanisha Rais Kenyatta na Naibu wake kwani uhasama kati yao unaweza kuvuruga uthabiti nchini.

“Kwa kutoelewana kuhusu masuala mengi haswa ya kisiasa, Rais Kenyatta na Dkt Ruto wanaibua wasiwasi miongoni mwa Wakenya, hali ambayo inaweza kuchochea ghasia za kisiasa,” maaskofu hao 23 wakasema kwenye taarifa na mwenyekiti wa Askofu Martin Kivuva, anayesimamia dayosisi ya Mombasa.

‘Tunahofu kwamba ikiwa uhasama kati ya Rais na Naibu wake itaigwa na wafuasi wao, utasababisha madhara makubwa nchini,” wakasema kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya KCCB, mtaani Karen, Nairobi.

Walisema kuwa taifa change kama Kenya linahitaji umoja baina ya viongozi wakuu ili liwezea kufikia malengo yake yake ya maendeleo kwa manufaa ya raia.

Lakini japo, Alhamisi Dkt Ruto alisema yu tayari kuridhiana na Rais, wiki jana wabunge wandani wake walisema hilo litawezekana tu baada ya masharti kadhaa kutimizwa.

Kwa mfano, wanataka Rais Kenyatta amerejeshee Dkt Ruto majukumu aliyompokonya na wabunge na maseneta wandani wake waliopokonywa nyadhifa za uongozi bunge walirejeshewe vyeo hivyo.

Uhasama kati ya Rais Kenyatta na Dkt Ruto ulianza baada ya Machi 9, 2018 Rais aliporidhiana kisiasa na aliyekuwa mpinzani wake mkuu Raila Odinga kupitia kile kinachotajwa kama ‘handisheki.”

You can share this post!

Aliyelaghai Sh5Milioni ashtakiwa

Munyes na Keter waitwa na Seneti kuhusu bei ya mafuta